1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robo ya watoto chini ya miaka 5 wana uhaba mkubwa wa chakula

Angela Mdungu
6 Juni 2024

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema kuwa robo ya watoto wote ulimwenguni wenye chini ya miaka mitano wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Watoto chini ya miaka 5 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula
Watoto wa Kipalestina wakisubiri kupewa chakula GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Taarifa hiyo inamaanisha kuwa, zaidi ya watoto milioni 180 kote duniani wako hatarini kupata athari zinazotokana na ukosefu wa chakula  katika ukuaji wao.

Kulingana na ripoti hiyo mpya ya Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF iliyochapishwa Jumatano, upungufu mkubwa wa chakula kwa watoto, unawagusa watoto wanaoishi kwa kupata milo dhaifu kupindukia na kuwa wanaishi kwa kutegemea makundi mawili pekee ya vyakula.

Soma zaidi: Watoto 68,000 Nepal wahitaji msaada

Akifafanua zaidi juu ya utafiti huo, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo Harriet Torlesse, amesema kuwa watoto 440 million wenye chini ya miaka mitano wanaoishi katika mataifa 100 yenye uchumi wa kati hawapati mlo kamili kila siku. Naye Mkuu wa shirika hilo la kuhudumia watoto Catherine Russell ameeleza kuwa watoto Milioni 181 kati ya milioni 440 waliotajwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hali inayosababisha wapate utapiamlo. 

Mataifa 20 yameathiriwa zaidi na upungufu wa chakula kwa watoto

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, umasikini wa upatikanaji wa chakula uliokithiri kwa watoto umejitokeza zaidi katika mataifa 20 yenye hali mbaya yakiwemo Somalia ambamo asilimia 63, wameathiriwa. Mataifa mengine ni Guinea  yenye asilimia 54 percent, Guinea-Bissau ikiwa imeathirika kwa asilimia 53 na athari ya hali hiyo kwa watoto huko Afghanistan ni asilimia 49.

Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa, katika Ukanda wa Gaza ambako jeshi la Israel linafanya mashambulizi baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, hali ya chakula na mfumo wa afya ni mbaya.

Misaada ya shirika la kiuto ya shirika la UNICEF kwa ajili ya Ukanda wa GazaPicha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Soma zaidi:Tatizo la Utapiamlo latishia kizazi kijacho cha Afghanistan 

Tangu mwezi Desemba mwaka jana  hadi Aprili mwaka huu  shirika  la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa limefanya awamu tano za ukusanyaji taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kutoka katika familia zinazopokea misaada kwenye eneo hilo. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa watoto tisa kati ya 10 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Lilibaini pia maendeleo madogo katika kushughulikia mzozo huo kwa muongo mmoja uliopita  na hivyo limetoa wito wa kutatuliwa kwa mzozo huo, kuboreshwa kwa huduma za jamii na misaada ya kiutu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupita kiasi.

UNICEF limeomba pia mfumo wa usindikaji wa chakula uboreshwe kote duniani, kwa kuwa vinywaji vyenye sukari nyingi na vyakula vilivyosindikwa kupitiliza vimekuwa vikitafutiwa masoko kwa fujo kwa wazazi. Limesema sasa imekuwa ni kawaida mpya kwa familia kuwalisha watoto vyakula hivyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW