ROMA: Waziri mkuu wa Italia asema kuna njama ya kutaka kumuua
3 Novemba 2005Waziri mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, amesema maisha yake yanalengwa katika shambulio la mtu wa kujitoa muhanga. Alisema katika mahojiano yake na gazeti la Libero nchini humo kwamba mshambuliaji wa kujitoa muhanga alitaka kumuua katika uwanja wa mpira wa San Siro mjini Milan.
Waziri Berlusconi anaimiliki timu ya soka ya AC Milan na mara kwa mara huenda kutazama michuano katika uwanja huo wa San Siro. Shirika la habari la ANSA limeripoti kwamba waendesha mashtaka wa mji wa Milan hawakuwa na habari zozote kuhusu njama dhidi ya waziri mkuu huyo katika uwanja wa San Siro.
Berlusconi aliyasema hayo katika juhudi za kutangaza msimamo wake juu ya Irak na katika mahojiano kwenye televisheni aliposema alijaribu kumshawishi rais George W Bush wa Marekani asiivamie Irak.