1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROME: Afya ya Papa imezidi kuzorota

1 Aprili 2005

Hali ya afya ya baba mtakatifu imechukua mkondo mpya ambapo hivi sasa baba mtakatifu yupo katika hali mahututi kufuatia homa kali iliyosababishwa na maambukizi katika njia ya kupitishia haja ndogo.

Baba mtakatifu hivi sasa anaangaliwa kwa karibu na madaktari wa Vatican huku akitibiwa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kituo cha runinga cha Marekani CNN maafisa wa Vatican wamesema hali ya baba mtakatifu ni mbaya sana na hivyo amepewa baraka za mwisho anazopewa mtu anayekaribia kufariki kulingana na utaratibu wa kanisa Katoliki .

Baba mtakatifu hadi kufikia wakati huu hajapelekwa hospitali kama ilivyo kawaida kutokana na kuwa hali yake ni dhaifu mno. Mamia ya waumini wa madhehebu ya kikatoliki waliokuwa wanabubujikwa na machozi walizingira makao makuu ya Vatican wakimuombea baba mtakatifu na kuwasha mishumaa.

Siku ya jumatano baba mtakatifu alichomekwa kijibomba chembamba cha kupitishia chakula kupitia puani ili kumsaidia kupata nguvu na kuponesha koo yake aliyofanyiwa upasuaji .Baba mtakatifu pia amewekwa kijibomba cha kumsaidia kupumua kwenye koo yake tangu kufanyiwa upasuaji huo. Baba mtakatifu mwenye umri wa miaka 84 pia anaugua ugonjwa wa kutetemeka.