ROME : Mustakbali wa serikali ya Italia mashakani
23 Februari 2007Rais Giorgio Napolitano wa Italia amekuwa na mazungumzo ya dharura kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Romano Prodi.
Prodi amejiuzulu baada ya serikali yake ya mseto ya mrengo wa shoto wa wastani kushindwa katika kura muhimu katika baraza la senate la bunge la Italia.Muswada huo ulioshindwa kupita ulijumuisha mipango ya kuongeza muda wa wanajeshi 2,000 wa Italia walioko nchini Iraq na Afghanistan na kuidhinisha utanuzi wa kambi ya kijeshi ya Marekani ilioko kwenye mji wa kaskazini wa Vicenza.
Rais Napolitano sasa inabidi aamuwe aidha kumuomba Prodi au kiongozi mwengine kuunda serikali mpya ya mseto au kuitisha uchaguzi mpya.
Rais huyo ameitaka serikali ya Prodi kuendelea kubakia madarakani kwa hivi sasa kutimiza dhima kama serikali ya mpito.