Ron DeSantis ajitosa katika mbio za urais wa Marekani 2024
25 Mei 2023Mahojiano hayo ya saa nzima ya mtandao wa Twitter yaliyoongozwa na mmliki wa jukwaa hilo la kijamii Elon Musk, ambayo yalilenga kutumika kama uzinduzi rasmi wa kampeni za DeSantis, yalikumbwa na matatizo ya kupotea sauti na maelfu ya watumiaji wakashindwa kujiunga au wakaondolewa. "Hakuna mbadala wa ushindi. Lazima tukomeshe utamaduni wa kushindwa ambao umeambukiza chama cha Republican katika miaka ya karibuni. Lazima tuangalie mbele, sio nyuma. Tunahitaji ujasiri wa kuongoza na lazima tuwe na nguvu ya kushinda."
Soma pia: Marekani: Ron DeSantis kutangaza nia ya kuwania urais
Kujitosa kwa DeSantis katika kinyang'anyiro cha tiketi ya Republican kunaweka mpambano mkali dhidi ya aliyewahi kuwa mshirika wake, Rais wa zamani Donald Trump, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais wa 2020 na Mdemocrat Joe Biden.
Gavana huyo wa Florida anajinadi kama afisa mkuu mtendaji aliyesimama kidete kuipinga serikali kuu kuhusu sera za UVIKO.
Soma pia: Biden atangaza kuwania tena urais wa Marekani
Alitetea sera zake jimboni Florida za kupiga marufuku ufundishaji wa dhana kama vile utambulisho wa kijinsia na ubaguzi wa kimfumo akisema ni njia ya kuwalinda Watoto wadogo. Katika siku za karibuni, alisaini hatua zinazozuia vikali utoaji mimba jimboni humo, zinazofanya kuwa rahisi kwa wakaazi kubeba silaha zilizofichwa miongoni mwa mambo mengine.
Huku wasifu wake ukiongozeka kitaifa na kile kinachotarajiwa kuwa rasimali nyingi za kifedha, DeSantis mwenye umri wa miaka 44, mara moja amekuwa mpinzani mkuu wa Trump kwa uteuzi wa tiketi ya Republican. Alionekana kumkosoa Trump isipokuwa hakumtaja moja kwa moja. "Pia tunaelewa kuwa kuongoza serikali sio burudani. Sio kujenga sifa yako au kutoa kauli za usahihi wa maadili, ni kuhusu kuleta matokeo. Na matokeo yetu jimboni Florida yamekuwa bora zaidi."
Trump, mwenye umri wa miaka 76, hakuchelewa kumkejeli DeSantis kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, kutokana na mwanzo wa kuyumba wa kampeni yake. Aliandika "Uzinduzi wa DeSanctus kwenye Twitter ni janga! Kampeni yake yote itakuwa janga.” Musk alikiri kuwepo matatizo ya kiufundi kwa sababu ya ukubwa wa hafla hiyo lakini akaongeza kuwa ni kitu kizuri sana kwa watu kusikia moja kwa moja kutoka kwa wagombea wa urais.
Mapema jana, DeSantis alijaza fomu katika tume ya uchaguzi ya Marekani. Gavana huyo anakabiliwa na kazi kubwa ya kuziba mwanya mkubwa wa umaarufu kati yake na Trump, huku Trump akiwa kifua mbele kwa karibu asilimia 40 ya pointi, licha ya kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kifedha na kupatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono katika kesi ya mjini New York.
Wagombea wengine wa Republican waliotangaza nia yao ni Pamoja na Nikki Haley, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, na Tim Scott, seneta wa Marekani kutoka South Carolina.
Mgombea mkuu wa Republican atakabiliana na Mdemocrat Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba 2024.
reuters, ape, afp