1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ronaldo akasirishwa kunyang'anywa taji na Modric

Sekione Kitojo
31 Agosti 2018

Christiano Ronaldo amekasirishwa na kunyang'anywa taji na mchezaji nyota MCroatia Luka Modric katika tuzo ya mchezaji bora wa mwaka  wa shirikisho la UEFA, amefichua hilo kocha wa Juventus Massimiliano Allegri.

Fussball Italien - Cristiano Ronaldo
Picha: picture-alliance/Pacific Press/A. Gandolfo

Mchezaji  wa  Real Madrid  na  Croatia  Modric  alimshinda  mchezaji mwenzake  wa  zamani  Ronaldo  pamoja  na  mshambuliaji  wa Liverpool Mohammed Salah  katika  tuzo  hiyo  ambayo  ilitolewa siku  ya  Alhamis  mjini  Monaco.

"Jana Ronaldo  alikuwa  amekasirika  sana , na  ni  kitu  cha kawaida,"  alisema  Allegri.

Cristiano Ronaldo Picha: Reuters/M. Sezer

"Alifunga  mabao 15 katika  Champions League  na  kushinda  kombe hilo  pamoja  na  wachezaji  wenzake . "Jinsi  Ronaldo alivyoichukulia  hali  hiyo  inaonesha  ni  vipi  anaendelea kupambana  na  kufanyakazi  kuwa  mchezaji  bora  kabisa. Hii  ni kwa  faida  yetu.

Allegri  aliongeza  kwamba  kumchagua  Modric  ni "uchaguzi  wa binafsi" wa  wale waliopiga  kura" na, kama  ni  hivyo  ni  lazima uheshimiwe."

ronaldo  mwenye  umri  wa  miaka  33, amepozwa  kidogo  baada  ya kuteuliwa  kupata  tuzo  ya mshambuliaji  bora  na  waandishi   habari na  makocha  wa  timu  zilizoshiriki  katika  Champions  League  na Ligi  ya  ulaya  kutoka  msimu  uliopita.

Mchezaji nyota wa Croatia na Real Madrid Luka ModricPicha: Getty Images/AFP/V. Vache

Mafanikio  ya  Modric , baada  ya  kuteuliwa  kuwa  mchezaji  bora katika  kombe  la  dunia, yana  maana  kwamba  mchezaji  huyo mwenye  umri  wa  miaka  32 anapaswa  kuwa  miongoni mwa wachezaji  wanaoweza  kutoroka  na  tuzo ya  mpira  wa  dhahabu Ballon d'Or, tuzo  ambayo  Ronaldo   na  Lionel Messi  walikuwa peke  yao  wakibadilishana  katika  muongo  mmoja  uliopita.

Ronaldo, mshindi  mara  tano  wa  tuzo  ya  mchezaji  bora  wa mwaka  duniani , alisainiwa  na  mabingwa  wa  Italia  Juventus msimu  huu kutoka  Real Madrid kwa  kitita  cha  euro milioni 100.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri : Idd Ssessanga