1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ronaldo: Fainali za Kombe la Dunia 2026 ni za mwisho kwangu

12 Novemba 2025

Cristiano Ronaldo amesema amebakiwa na mwaka mmoja ama miwili ya kusakata kabumbu na kuongeza kuwa fainali ya michuano ya Kombe la Dunia 2026 zitakuwa ndio za mwisho.

Saudi Pro League 2025 | Al Hilal dhidi ya Al Nassr | Cristiano Ronaldo wa Al Nassr
Cristiano Ronaldo wa Al Nassr akishangilia baada ya kufunga bao wakati wa mechi ya Ligi ya Saudi Pro kati ya Al Hilal dhidi ya Al Nassr katika Uwanja wa Kingdom mnamo Aprili 04, 2025 huko Riyadh, Saudi Arabia.Picha: Mohammed Saad/Anadolu/ABACA/picture alliance

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno aliulizwa juu ya hatima yake kwenye soka katika mahojiano kwa njia ya video kwenye tukio la TOURISE Riyadh siku ya Jumanne.

Amesema kwenye kipindi cha Piers Morgan Uncensored wiki iliyopita kwamba atatundika daluga "hivi karibuni." Lakini kabla ya kuthibitisha, alitania kwa kusema "hivi karibuni... namaanisha pengine ni baada ya miaka 10", kabla ya kuongeza kuwa "Ninaposema hivi karibuni.. ninamaanisha nafurahia sana wakati nilionao sasa. Kama mnavyojua kwenye soka ukishafika umri fulani unabakia kuhesabu miezi haraka haraka.

"Kwa hiyo nafurahia wakati huu, najisikia vizuri sana, ninafunga magoli, nina kasi kubwa, nafurahia kucheza kwenye timu yangu ya taifa na klabu ya Al Nassr, lakini kwa ujumla tuwe tu wakweli, ninaposema 'hivi karibuni' pengine ni mwaka mmoja ama miwili ya kuendelea kucheza."

Cristiano Ronaldo wa Ureno akinyanyua kombe la Ligi ya Mataifa ya UEFA baada ya ushindi wa timu yake katika mchezo wa fainali wa Ligi ya Mataifa ya UEFA 2025 kati ya Ureno na Uhispania katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Munich mnamo Juni 08, 2025 huko Munich, Ujerumani.Picha: Alexander Hassenstein/Getty Images

Alipoulizwa ikiwa hiyo inamaanisha kwamba Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakuwa ndio za mwisho, alijibu: "Kabisa, ndio, kwa sababu nitakuwa na miaka 41 na ninadhani wakati utakuwa umefika, nikiwa kwenye michuano mikubwa.

Kama nilivyokwambia hapo kabla, ninafurahia wakati nilionao, lakini ninaposema hivi karibuni, ni karibuni kwelikweli kwa sababu ninajitoa kwa kila hali kwenye soka. Nipo kwenye soka tangu miaka 25 iliyopita, nilifanya kila kitu, nina rekodi nyingi za aina mbalimbali, kuanzia kwenye klabu hadi timu ya taifa.

Kombe la Dunia ndilo pekee na kubwa zaidi ambalo Ronaldo hajawahi kushinda akiwa na timu yake ya taifa. Ameshinda tu Kombe la Euro akiwa na kikosi hicho, mwaka 2016. Cristiano Ronaldo mwezi Juni alisaini mkataba mpya wa miaka miwili na klabu ya Al Nassr.  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW