Rouhani asema Marekani itajuta ikijitoa mkataba wa nyuklia
6 Mei 2018"Ikiwa Marekani itaondoka kwenye makubaliano ya nyuklia, mutaona hivi karibuni watakavyojutia kuliko ilivyowahi kuwatokezea kwenye historia," alisema mwanamageuzi Rouhani kwenye hotuba yake ya leo (Jumapili 6 Mei) akiwa kaskazini mwa Iran.
"Trump anapaswa kujuwa kuwa watu wetu wameunganika, utawala wa Kizayuni (Israel) unapaswa kujuwa kuwa watu wetu wako kitu kimoja," alisema Rouhani.
"Leo, mirengo yote ya kisiasa nchini Iran, ama iwe kulia au kushoto, wahafidhina, wanamageuzi na watu wa mrengo wa kati, wote wameungana," aliongeza.
Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kujiondoa kwenye makubaliano hayo wakati utakapofika muda wa kusainiwa upya tarehe 12 Mei, akiwataka washirika wa Ulaya "kuyarekebisha makosa makubwa yaliyomo" ama sivyo arejeshe upya vikwazo dhidi ya Iran.
Mkataba huo wa nyuklia ulisainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani, wakati huo ikiongozwa na Barack Obama.
Chini ya makubaliano hayo, vikwazo vilipunguzwa kwa masharti ya Iran kutokuunda bomu la nyuklia, lakini Iran inasema haioni mafanikio ya ahadi hizo licha ya kutimiza masharti ya mkataba.
Mara kadhaa, Rouhani amekuwa akirejelea msimamo wa nchi yake kupinga kuzuiliwa nchi yake kuunda makombora yasiyo ya kinyuklia, na hilo amelizungumzia pia kwenye hotuba yake ya Jumapili.
Naye Trump amekuwa akiukosoa mkataba huo, akitaja baadhi ya vifungu ambavyo anasema vinaondoa vikwazo vya nyuklia kuanzia mwaka 2025.
Macron aonya dhidi ya vita
Katika jitihada za kuyaokoa makubaliano hayo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amependekeza hivi karibuni kwamba mkataba huo utanuliwe kuyashirikisha masuala kama hayo yanayolalamikiwa na Trumo, na pia kuondoa kikomo ya muda wa Iran kuruhusiwa kuunda makombora mengine na pia kuangalia dhima ya Iran kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.
Hatua ya Iran kumuunga mkono Rais Bashara al-Assad, kupitia kundi la Hizbullah la Lebanon, na pia kuwaunga mkono waasi wa Kishia nchini Yemen kumeongeza mzozo kati yake na mataifa ya Magharibi.
Licha ya hayo, hivi leo Rais Macron ameonya kwamba kunaweza kuzuka vita endapo marekani itajiondoa kwenye makubaliano hayo.
"Tunaweza kuibuwa mambo mengine mapya. Kunaweza kukawa na vita," Macron ameliambia gazeti la kila wiki la Ujerumani, Der Spiegel, ingawa ameongeza: "Sidhani kama Donald Trump anataka vita."
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Zainab Aziz