Rouhani ataka kupanua uhuru wa watu binafsi Iran
8 Januari 2018Taarifa kamili na Sekione Kitojo.
Kiongozi huyo , ambaye alimshinda mgombea ambaye ni mwenye msimamo mkali wa kupinga mataifa ya magharibi na kushinda uchaguzi mpya mwaka , pia alitoa wito wa kuondolewa kwa vizuwizi katika mitandao ya kijamii inayotumiwa na waandamanaji wanaoipinga serikali katika changamoto kubwa ya muda mrefu kwa maafisa wenye msimamo mkali tangu mwaka 2009.
"ilikuwa ni uwasilishaji usiofaa wa matukio na pia tusi kwa watu wa Iran kusema walikuwa tu na madai ya kiuchumi," Rouhani alinukuliwa akisema na shirika la habari la Tasnim.
"watu walikuwa na madai ya kiuchumi, kisiasa na kijamii."
Jeshi la Iran lenye ushawishi mkubwa la mapinduzi , lilisema jana Jumapili kuwa majeshi ya usalama yamefikisha mwisho machafuko ya wiki nzima yaliyochochewa na kile ilichosema maadui ya nje.
Maandamano, ambayo yalianza kuhusiana na ugumu wa maisha yanayowakumba vijana na tabaka la wafanyakazi, yalisambaa hadi katika zaidi ya miji 80 na yalisababisha vifo vya watu 22 na zaidi ya wengine 1,000 walikamatwa, kwa mujibu wa maafisa nchini Iran. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif amesema ni wazo lisilokubalika kwa nchi jirani kuidhoofisha nchi yake.
Hakuna nchi inaweza kujipatia usalama pekee yake kwa kuidhoofisha nchi jirani. Ni wazo la hatari katika duniani hii ya utandawazi.
Viongozi wa mandamano wametambuliwa
Hamid Shahriari , naibu mkuu wa mahakama alisema kwamba viongozi wote wa maandamano wametambulika na kukamatwa, na wataadhibiwa vikali na huenda wakakabiliwa na adhabu ya kifo.
Mbunge mmoja wa Iran amethibitisha leo kifo cha mmoja kati ya wafungwa waliokamatwa.
"Kijana huyo wa miaka 22 alikamatwa na polisi. Nilifahamishwa kwamba alijiua akiwa jela, " Tayebeh Siavashi alinukuliwa akisema na shirika la habari la ILNA.
Waandamanaji wengi walihoji sera za mambo ya kigeni za Iran katika mashariki ya kati , ambako nchi hiyo inaingilia nchini Syria na Iraq katika vita kwa ajili ya kujipatia ushawishi dhidi ya hasimu wake Saudi Arabia.
Msaada wa kifedha kwa Wapalestina na kundi la Washia la Lebanon pia umewakasirisha Wairani, ambao wanataka serikali yao kuaangalia zaidi kuhusu matatizo ya ndani badala ya kusaidia mataifa ya nje.
Akirejea baadhi ya matamshi yake katika kampeni, Rouhani alisema leo kwamba watu wanapaswa kuruhusiwa kuwakosoa maafisa wote wa Iran , bila kubagua.
Awali waandamanaji walielekeza hasira yao kuhusiana na bei ya juu ya bidhaa pamoja na madi ya kuwapo na rushwa , lakini maandamano hayo yalichukua mkondo mwingine wa kisiasa , ambapo idadi kubwa ya watu walimtaka kiongozi mkuu wa kidini nchini humo Ayatollah Ali Khamenei ajiuzulu.
Kiongozi huyo mkuu ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na anateua viongozi wa mahakama.Mawaziri muhimu wateuliwa kwa makubaliano nae na ana kauli ya mwisho kuhusiana na sera za mambo ya kigeni ya Iran. Kwa ulinganisho , rais ana madaraka madogo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman