Rouhani iataka Japan kufanya upatanishi na Marekani
20 Desemba 2019Rouhani , akiwa ni rais wa kwanza wa Iran kufanya ziara nchini Japan katika kupindi cha miaka miaka 19, alimwambia waziri mkuu Shinzo Abe kuwa makubaliano ya nyuklia na mataifa makubwa duniani bado ni muhimu.
"Makubaliano ya nyuklia bado ni muhimu sana kwa Iran. Kwa hiyo nashutumu vikali kujitoa kwa Marekani ambako ni kwa upande mmoja na bila sababu. Nina matumaini Japan na mataifa mengine yatafanya juhudi kuendeleza makubaliano haya."
Abe katika matamshi yake ya ufunguzi, ameitaka Iran kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo na kuchukua juhumu muhimu katika kufanikisha amani na uthabiti katika eneo hilo. Abe ameeleza wasi wasi wake juu ya kuongezeka kwa hali ya wasi wasi katika mashariki ya kati na kuahidi kuchukua hatua zaidi kadri inavyowezekana kulisaidia eneo hilo kudumisha uthabiti.
"Nina matumaini makubwa kuwa Iran itatekeleza kikamilifu makubaliano ya nuklia, na kuchukua jukumu muhimu katika kuhimiza amani na uthabiti kwa ajili ya kanda hiyo ya mashariki ya kati."
Eneo la Mashariki ya kati linaipatia Japan kiasi cha asilimia 80 ya mafuta. Japan , ambayo ni mshirika wa Marekani ambae ana mahusiano ya kiasili na Iran , pia inataka kuchukua jukumu la kuwa mpatanishi kati ya Tehran na Washington. Abe amesema kuwa jukumu kama hilo linatarajiwa na jumuiya ya kimataifa.
Rouhani , ambaye alikuwa nchini Malaysia kuhudhuria mkutano wa mataifa ya Kiislamu, aliwasili mjini Tokyo leo Ijumaa mchana kwa ziara itakayomchukua siku nzima na kukutana na Abe na kula nae chakula cha usiku, kwa mujibu wa maafisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Japan.
Hali ya wasi wasi imeongezeka kati ya Iran na marekani tangu pale rais Donald Trump kuchukua uamuzi mwaka jana kuiondoa nchi yake kutoka katika makubaliano ya kinyuklia na Iran mwaka ya mwaka 2015.