1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rouhani: Marekani imekosea kuhusu jeshi la mapinduzi

9 Aprili 2019

Rais wa Iran Hassan Rouhani ametetea kikosi cha ulinzi wa mapinduzi cha taifa hilo, siku moja baada ya Marekani kukiorodhesha kuwa kundi la nje la kigaidi. Rais Donald Trump amekitaja kikosi hicho kuwa kundi la kigaidi.

Iran Revolutionsgarden in Teheran
Picha: Getty Images/AFP

Rais wa Marekani Donald Trump, siku ya Jumatatu aliliorodhesha jeshi la walinzi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kuwa kundi la kigaidi la kigeni -- katika hatua ya kihistoria itakayochochea wasiwasi katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Uhusiano kati ya Tehran na Washington ulichukuwa mkondo mbaya zaidi mwezi Mei mwaka uliopita wakati Trump alipotangaza kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya mataifa sita makubwa duniani pamoja na Iran, na kurejsha vikwazo vikali dhidi ya taifa hilo.

"Walinzi hao wamejitolea maisha yao kulinda watu wetu, mapinduzi yetu (ya Kiislamu ya 1979) .... Lakini leo, Marekani ambayo ina kinyongo dhidi ya jeshi hilo, imewaorodhesha walinzi kuwa magaidi," alisema Rouhani katika hotuba iliyotangazwa mubashara kwenye televisheni ya taifa.

Tehran ilichukuwa hatua za kulipa kisasi kwa kuitangaza kamandi kuu ya jeshi la Marekani (CENTCOM) kama kundi la kigaidi na serikali ya Marekani kama mfadhili wa ugaidi, na maafisa wa Iran walionya kuwa hatua hiyo itahatarisha maslahi ya Marekani katika eneo hilo, ambako Iran inashiriki vita vya uwakala kuanzia Syria hadi Lebanon.

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema Marekani lifanya kosa kubwa kukiorodhesha kikosi cha walinzi wa mapinduzi kuwa kundi la kigaidi.Picha: Reuters/S. Chirikov

"Kosa hili litawaunganisha Wairan na walinzi wa mapinduzi watazidi kuwa mashuhuri nchini Iran na kwenye kanda...Marekani imetumia magaidi kama zana katika kanda hiyo huku walinzi wa mapinduzi wamepigana nao kuanzia Iraq hadi Syria," alisema Rouhani.

Makamanda wa vikosi vya ulinzi wa mapinduzi wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba vituo vya jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na meli za kivita za Marekani katika Ghuba viko ndani ya umbali wa makombora ya Iran.

Tehran pia imetishia kuvuruga usafirishaji wa mafuta kupitia njia ya bahari ya Hormuz katika kanda ya Ghuba ikiwa Marekani itajaribu kudhoofisha uchumi wake kwa kusitisha mauzo yake ya mafuta.

Hasimu mkuu wa Iran Saudi Arabia imekaribisha uamuzi wa Marekani siku ya Jumanne. Taifa hilo la kifalme la Kisunni na Iran inayofuata madhehebu ya Kishia yamekuwa yakipigana vita vya uwakala kwa miaka kadhaa, yakiunga mkono pande hasimu katika migogoro nchini Syria na Yemen, na Riyadh inaituhumu Tehran kwa kuingilia masuala yake ya ndani pamoja ya mataifa mengine ya mataifa ya Mashariki ya Kati.

"Uamuzi wa Marekani unafasiri matakwa ya mara kwa mara ya ufalme kwa jamii ya kimataifa kuhusu umuhimu wa kukabiliana na ugaidi unaofadhiliwa na Iran," lilisema shirika la habari la Saudi Arabia SPA, likinukuu duru kutoka wizara ya mambo ya nje.

Baadhi ya asakri wa kikosi cha walinzi wa mapinduzi wakiwa kwenye gwaride.Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

"Uvumilivu wetu una mipaka"

Katika kuonyesha mshikamamo, wabunge wa Iran walivaa sare za kikosi cha ulinzi wa mapinduzi kwenda bungeni siku ya Jumanne, wakighani "kifo kwa Amerika" wakati Ira ikiadhimisha siku ya kitaifa ya kila mwaka ya walinzi wa mapinduzi, liliripoti shirika la habari la Fars.

"Uamuzi wa Marekani kuliorodhesha jeshi la walinzi wa mapindizi kama kundi la kigaidi ndiyo ulikuwa kilele cha upumbavu na ujinga wa uongozi wa Marekani," shirika la Fars lilimnukuu spika wa bunge Ali Larijani akisema.

Iran mpaka sasa imeendela kuheshimu makubaliano ya nyuklia lakini watawala wa kidini mjini Tehran wametishia kujitoa katika makubaliano hayo na kurudi kwenye mpango wao waliousitisha wa kurutubisha nyuklia ikiwa mataifa mengi yaliosaini makubaliano hayo yatashindwa kulinda maslahi ya Iran.

"Nawaambia nyinyi (viongozi wa Marekani), ikiwa mtatushinikiza, tutatengeneza kwa wingi mitambo ya IR8," alisema Rouhani katika hotuba ya kuadhimisha siku ya taifa ya nyuklia ya Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amezionya kampuni na benki kote duniani dhidi ya kufanya biashara na kikosi cha walinzi wa mapinduzi cha Iran.Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Chini ya makubaliano ya nyuklia, vikwazo vilivyowekwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa viliondolewa baada ya iran kukubali kusiitsha uendelezaji wa muda mrefu wa mpango wake wa nyuklia ambao mataifa ya Magharibi yalishuku ulilenga kutengeneza bomu la atomiki.

Utawala wa Trump unasema makubaliano hayo ya nyuklia hayakufika mbali vya kutosha kuzuwia uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya mataifa ya kanda au kudhibiti mpango wake wa utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.

Mataifa mengine yaliosaini makubaliano hayo, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yanajaribu kunusuru makubaliano hayo na mwezi Januari yalianzisha mfumo unaoruhusu biashara na Tehran na kukwepa vikwazo vya Marekani.

Lakini Iran imeukosoa Umoja wa Ulaya kwa kushindwa "kuheshimu ahadi zake" za kulinda biashara na Iran. Rouhan, ambaye anaweza kudhoofishwa na na pigo kwa uchumi wa Iran ikiwa makubaliano hayo yatasambaratika, alitumia maneno makali katika hotuba yake ya televisheni.

"Tumekuwa wavumilivu na tutaendelea kuwa wavumilivu...lakini uvumilivu wetu una kikomo....Timizeni ahadi zenu na heshimuni ahadi," Rouhani aliuambia Umoja wa Ulaya.

chanzo.rtre

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW