RSF: Tuko tayari kutekeleza mpango wa usitishwaji mapigano
27 Septemba 2024Mkuu wa kikosi cha RSF nchini Sudan Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, amesema kundi hilo liko tayari kutekeleza mpango wa usitishaji vita kote nchini humo ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
Kiongozi huyo wa RSF ameitoa kauli hiyo mbele ya mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, baada ya Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, kuwatuhumu wanamgambo hao kuzuia juhudi za amani.
Soma: Pande hasimu nchini Sudan zakubali mazungumzo ya kusaka amani
Al-Burhan amelitolea pia wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitambua RSF kama kundi la kigaidi, akisema wanaendesha mauaji ya kikabila, kuwalazimisha watu kuyahama makazi yao pamoja na mauaji ya halaiki.
Hayo yanaripotiwa wakati mapigano makali yameendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini Sudan ikiwa ni pamoja na mji mkuu Khartoum na mji wa Omdurman.