RSF: Waandishi 54 waliuawa wakiwa kazini mwaka 2024
12 Desemba 2024Matangazo
Ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo iliyotolewa leo, imeeleza kuwa theluthi moja ya waandishi hao wameuawa katika Ukanda wa Gaza.
RSF imesema hadi sasa idadi ya waandishi habari waliouawa, kulingana na takwimu za mwishoni mwa mwezi Novemba, ziko sawa na kiwango cha mwaka uliopita.
Shirika hilo limesema kuripoti kuhusu vita ni hatari sana, na kwamba waandishi habari 31 kati ya 54 waliuawa katika maeneo yenye mizozo.
Kulingana na RSF, idadi hiyo ni kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano.
RSF imekuwa ikiitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, ikiwezekana iyachunguze mauaji ya wafanyakazi wa vyombo vya habari kama uhalifu wa kivita.