RSF wakubali makubaliano ya amani ya kibinadamu
7 Novemba 2025
Wapiganaji wa kikosi cha Rapid Support Forces RSF nchini Sudan, wametangaza jana Alhamisi kwamba wamekubali pendekezo la makubaliano ya amani ya kibinadamu yaliyotolewa na nchi nne wapatanishi, Marekani, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia.
Tangazo hili linafuatia hatua ya RSF kuuteka kwa mji mkubwa muhimu wa El-Fasher, ambayo ililiondoa jeshi kutoka ngome yake ya mwisho katika eneo kubwa la magharibi mwa Darfur.
Tangu wakati huo wameshutumiwa kwa mauaji ya halaiki, uporaji na unyanyasaji wa kijinsia huko, na katika siku za hivi karibuni wameonekana kuelekeza nguvu na umakini wao katika eneo jirani la Kordofan, ambapo mapigano makali yanaendelea.
Serikali inayoungwa mkono na jeshi haikutoa kauli mara moja kuhusu tangazo la RSF.
Mapema jana, mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alisema vikosi vyake bado vinaendelea kujitahidi kumshinda adui.