RSF yachukua udhibiti wa mji wa Wad Madani
21 Desemba 2023Umoja wa Mataifa umeonya juu ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu mjini humo. Haya yanajiri wakati Shirika la Mpango wa Chakula WFP likitangaza kusitisha kwa muda msaada wa chakula katika baadhi ya maeneo ya Sudan.
Soma pia: Jeshi la Sudan lasema vikosi vyake vimeondoka Wad Madan
Vikosi vya wanamgambo wa RSF vimeongeza kasi katika wiki za hivi karibuni, vikiimarisha udhibiti wake kwenye eneo kubwa la Darfur na kutwaa maeneo mapya upande wa mashariki kueleke mji mkuu Khartoum.
Wad Madani ni mji mkubwa ulio takriban kilomita 170 kusini mashariki mwa Khartoum ambao umetumika kama kitovu cha misaada na kimbilio la wakimbizi wa ndani. Ni mji mkuu wa Jimbo la El Gezira, eneo muhimu la kilimo katika nchi hiyo inayokabiliwa na njaa inayozidi kuwa mbaya.
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kuingia kwa RSF mjini humo kumesababisha hadi watu 300,000 kukimbia makaazi yao, huku wakaazi wa mji wa Darfur wakisema kwamba mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi yamesababisha majeruhi miongoni mwa raia.
Soma pia: UNICEF yaomba dola bilioni 9.3 za kusaidia watoto 2024
Hofu ya ukikwaji wa haki
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani siku ya Jumanne ilitoa taarifa ikisema inasikitishwa sana na ripoti kwamba ndege za jeshi zilikuwa zikilipua maeneo yenye watu wengi kaskazini na kusini mwa Darfur.
Mkuu wa Haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema katika taarifa kuwa ana wasiwasi kufuatia ripoti za ukiukaji wa haki za binaadamu katika siku za karibuni kufuatia mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF.
Aidha Turk, ameelezea hofu iliyopo kuhusu hali mbaya ya kiutu katika Jimbo zima la Al-Gezira, ambalo linawahifadhi karibu watu nusu milioni waliopoteza makazi yao nchini Sudan.
RSF, ambayo imeshutumiwa kwa uporaji mkubwa, kuweka watu kizuizini na unyanyasaji wa kijinsia huko Khartoum na miji mingine, imesema kwamba itatoa ulinzi na huduma za kimsingi kwa raia huko Wad Madani.
Huku haya yakijiri Shirika la Mpango wa Chakula WFP limesema kwamba limesitisha msaada wa chakula kwa muda katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Gezira wakati mapigano yakienea kusini na mashariki mwa mji mkuu Khartoum.
Soma pia: Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF waendelea kushambuliana
Licha ya hali hiyo mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Eddie Rowe amesema wafanyakazi wa shirika hilo wanaendelea kujitahidi kutoa msaada wa chakula katika maeneo ambayo bado yanaweza kufikiwa.