RSF yatuhumiwa kuua watu wengi na kuficha uhalifu Sudan
20 Januari 2026
Naibu mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, ameliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kufanyika mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Kundi la RSF limetuhumiwa kuendesha mauaji hayo na kujaribu kuyaficha kwa kuwazika watu kwenye makaburi ya pamoja.
Jana Jumatatu kilifanyika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New-York, Marekani na naibu mwendesha mashtaka wa ICC Nazhat Shameem Khan alishiriki kwa njia ya video, kutokana na kunyimwa visa ya kwenda Marekani.
Katika ripoti yake mbele ya kikao hicho alifafanuwa kwa kina namna mauaji ya watu wengi yanavyofanyika katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Khan alikiiambia kikao hicho kwamba kwa mujibu wa tathmini iliyoendeshwa na ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu umefanyika katika mji wa El Fasher, kundi la wanamgambo wa RSF lilipoudhibiti mji huo mnamo mwezi Oktoba mwaka jana. Sudan
''Ubakaji, watu kushikiliwa jela kinyume cha sheria, mauaji, makaburi ya watu waliozikwa kwa pamoja, yote hayo yamefanyika kwa kiwango kikubwa, kwa sehemu kubwa uhalifu huu umerekodiwa na kushangiliwa na wale waliokuwa wakiutekeleza. Na hali hii ya kutisha bado inaendelea.''
Kwa mujibu wa tathmini yao mauaji ya watu wengi yamefanyika na pia juhudi za kuficha uovu huo. Video zilizopitiwa na ICC kwa mujibu wa Khan zinaonesha namna wanamgambo wa RSF walivyokuwa wakiwakamata raia kuwafanyia dhulma na kuwauwa katika mji wa El Fasher na kisha kushangilia matukio hayo ya kuua na kuzidhalilisha maiti.
Yote hayo Khan amesema, yako kwenye ushahidi uliokusanywa kupitia jamii zilizoathirika,sambamba na ushahidi uliowasilishwa na mashirika ya kiraia na wadau wengine.
Hofu yaongezeka Sudan baada ya waasi wa RSF kuuteka mji wa El Fasher
Tangu mwezi Aprili mwaka 2023 vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi la Sudan na Wanamgambo wa RSF vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha wengine milioni 11 bila makaazi na kuacha mgogoro mkubwa duniani wa baa la njaa na wasiokuwa na makaazi.
Naibu mwendesha mashtaka wa ICC Nazhat Shameen Khan ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana kwamba hali bado inatisha kwenye jimbo la Darfur ambalo linadhibitiwa na RSF.
''Hali katika jimbo la Darfur imezidi kuwa mbaya. Wakaazi wa eneo hilo hivi tunavyozungumza wanakabiliwa na mateso ya jumla jamala. Kuanguka kwa mji wa El Fasher mikononi mwa RSF kumekuwa kukiandamana kampeni iliyoratibiwa ya kuendesha mateso makubwa, ikiwalenga hasa, jamii za wasiokuwa na asili ya Kiarabu''
Katika vita hivyo vya nchini Sudan pande zote mbili jeshi na wanamgambo wa RSF wamekuwa wakituhumiwa kuendesha mauaji ya raia.
Zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu
Lakini kwa upande mwingine Jumatatu 19.01.2026 wanamgambo wa RSF walitangaza kusitikishwa na kile walichokiita mapigano ambayo hayakudhamiriwa kati yao na wanajeshi wa Chad, katika eneo la mpakani. Chad ilisema wanajeshi wake 7 waliuwawa kwenye tukio hilo.
Tamko la RSF kupitia mtandao wao rasmi wa Telegram lilifafanuwa zaidi kwa kusema kwamba mapigano hayo yalikuwa ni kosa ambalo halikudhamiriwa kutokea katika operesheni yao ya kijeshi.