Trump asema rubani wa Marekani apatikana hai Iran
5 Aprili 2026
Uokoaji wa mwanajeshi wa anga ulifanyika baada ya operesheni ya dharura ya utafutaji na uokoaji ya Marekani kufuatia ajali ya Ijumaa ya ndege ya kivita chapa F-15E Strike Eagle, huku Iran ikiahidi zawadi kwa yeyote ambaye angemkamata "rubani adui."
Rais wa Marekani Donald Trump alisema mwanajeshi huyo amejeruhiwa lakini yuko katika hali tulivu.
"Shujaa huyu alikuwa nyuma ya uwanja wa vita katika milima hatari ya Iran, akiwindwa na adui zetu ambao walikuwa wakimkaribia kila saa," Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
Mwanajeshi mwingine wa pili aliokolewa mapema. Ndege hiyo ya kivita ilikuwa ya kwanza ya Marekani kuanguka katika ardhi ya Iran tangu Marekani na Israel walipoanzisha vita kwa kuishambulia Iran tarehe 28 Februari.
Tangu wakati huo, vita vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, kutikisa masoko ya dunia, kukata njia muhimu za usafirishaji na kupandisha bei za mafuta. Pande zote mbili zimetishia na kushambulia malengo ya kiraia, jambo ambalo limeibua tahadhari kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita.
Hadi Jumapili (05.04.2026) Iran haikuonyesha dalili zozote za kurudi nyuma, ikilishambulia malengo mapya ya kiuchumi na miundombinu katika nchi jirani za Kiarabu za Ghuba.
Vitisho vya Trump kwa Iran
Trump alisema wiki iliyopita kwamba Marekani imeiangamiza Iran "kabisa" na ingewamaliza "haraka sana." Siku mbili baadaye, Iran iliangusha ndege mbili za kijeshi za Marekani, ikionyesha hatari zinazoendelea za kampeni ya mabomu na uwezo wa jeshi la Iran, ingawa limepungua nguvu, kuendelea kushambulia tena.
Kadiri Iran inavyoendelea kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, Trump, katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, alitishia kufungua "jahanamu yote" ikiwa hautafunguliwa kufikia Jumatatu.
Trump amewahi kutoa vitisho kama hivyo hapo awali na kuviongeza wakati wapatanishi walipodai kuwa kumekuwa na maendeleo ya kuhitimisha vita kwa makubaliano.
Ndege nyingine iliyoanguka ilikuwa ndege ya mashambulizi ya Marekani aina ya A-10. Hali ya wahudumu wake au mahali ilipoangukia haikujulikana mara moja. Jumapili, televisheni ya taifa ya Iran ilirusha video ikionyesha moshi mzito mweusi ukipanda hewani, ikidai kuwa wameidungua ndege ya usafiri ya Marekani na helikopta mbili zilizokuwa sehemu ya operesheni ya uokoaji.
Hata hivyo, afisa mmoja wa ujasusi wa kikanda aliyepewa taarifa kuhusu operesheni hiyo aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba jeshi la Marekani lilizilipua ndege mbili za usafiri kutokana na hitilafu ya kiufundi, na kulazimika kuleta ndege nyingine kukamilisha uokoaji. Afisa huyo alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na siri ya operesheni hiyo.
Droni za Iran zashambulia miundombinu ya nishati ya Ghuba
Huko Kuwait, shambulio la ndege isiyo na rubani la Iran lilisababisha uharibifu mkubwa kwa vituo viwili vya umeme na kukatiza huduma ya kituo cha kusafisha maji ya chumvi. Kulingana na Wizara ya Umeme, hakuna majeruhi walioripotiwa.
Na nchini Bahrain, kampuni ya kitaifa ya mafuta ilisema shambulio la droni lilisababisha moto katika kituo chake cha kuhifadhia mafuta, ambao ulizimwa. Uharibifu ulikuwa bado unakadiriwa na hakuna majeruhi waliothibitishwa.
Katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), mamlaka zilishughulikia milipuko kadhaa ya moto katika kiwanda cha petrokemikali cha Borouge.
Shambulio hilo lilitokea siku moja baada ya Israel kushambulia kiwanda cha petrokemikali nchini Iran ambacho Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kinaisaidia Iran kufadhili vita.
Wapatanishi kutoka Pakistan, Uturuki na Misri walikuwa wakifanya kazi kuzikutanisha pande hizo mbili (Marekani na Iran) mezani, kulingana na maafisa wawili wa ukanda huo.
Mpango wa kusitisha mapigano unajumuisha kusitishwa kwa uhasama ili kuruhusu suluhisho la kidiplomasia, kulingana na afisa wa ukanda aliyehusika na jitihada hizo pamoja na mwanadiplomasia wa Ghuba.