1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Rubio: Dunia ichukue hatua kukata njia za silaha kwa RSF

13 Novemba 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kukomesha usambazaji wa silaha kwa wanamgambo wa RSF akitaja hali nchini Sudan kuwa janga la kibinadamu lisilovumilika.

Sudan Khartoum 2025 | Jeshi la Sudan |
Mwanajeshi wa Sudan akikagua ghala la silaha lililogunduliwa mjini Khartoum, SudanPicha: AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha usambazaji wa silaha kwa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), akikitaja kuwa chanzo kikuu cha umwagaji damu unaoendelea nchini Sudan.

Rubio amesema kuwa RSF haina uwezo wa kutengeneza silaha ndani ya Sudan, na hivyo hutegemea msaada wa kifedha na vifaa kutoka nje ya nchi.

Ameongeza kuwa wanajua ni nchi gani inahusika na usambazaji huo, na kwamba Marekani itafanya mazungumzo na taifa hilo ili kulifahamisha juu ya athari za maamuzi yake kwa taswira ya kimataifa.

Ingawa hakuitaja moja kwa moja Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), mshirika wa karibu wa Marekani, jeshi la Sudan limeituhumu UAE kwa kuwapatia RSF silaha na mamluki kupitia mataifa kadhaa ya Afrika.

UAE, kwa upande wake, imekanusha vikali tuhuma hizo ikisisitiza kutohusika na mzozo unaoendelea Sudan kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF.