1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubio asema msaada wa Marekani kwa Israel "hautayumba"

23 Januari 2025

Waziri mpya wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesisitiza "uungaji mkono usioyumba" wa Washington kwa Israel siku kadhaa tangu kuanza kutekelezwa kwa makubaliano legelege ya kusitisha vita vya Gaza.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio. Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani aliyeapishwa siku mbili zilizopita baada ya kurejea madarakani kwa Donald Trump ametoa matamshi hayo alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, usiku wa kuamkia leo.

Kwenye mazungumzo hayo, Rubio amemhakikishia Netanyahu kwamba Washington itaendelea kusimama bega kwa bega na Israel na hilo ni kipaumbele cha juu cha rais Trump.

Pia amempongeza Netanyahu kwa kile amekiita kuwa mafanikio makubwa ya kuyasambaratisha makundi ya Hamas na Hezbollah na kumuahidi kwamba Marekani itafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha mateka wote wa Israel wanaoshikilishwa na Hamas wanaachiwa huru.

Israel na kundi la Hamas walianza kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano Jumapili iliyopita ambayo yanajumuisha kubadilishana wafungwa na mateka. Tayari mateka kadhaa wa Israel walikwishaachiwa huru na makumi ya wafungwa wa Kipalestina walitolewa kutoka jela za Israel.

Uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Ukingo wa Magharibi wateteresha utulivu 

Mwanamke wa Kipalestina akikatisha katikati ya magari ya kijeshi ya Israel yaliyo sehemu ya uvamizi wa kijeshi wa Israel katika mji wa Jenin huko Ukingo wa Magharibi.Picha: AFP

Wakati Rubio akizungumza na Netanyahu, Israel ilikuwa inaendelea na oparesheni yake ya kijeshi kwenye eneo la Wapalestina la Ukingo wa Magharibi.

Jeshi la Israel limesema limefanikiwa kuwaangamiza wale iliowataja kuwa "magaidi 10", wakati wizara ya afya ya Palestina imearifu kwamba operesheni hiyo iliyopachikwa jina la "Ukuta wa Chuma" imewaua watu 10 na kuwajeruhi wengine 35.

Gavana wa mji wa Jenin, ambako ndiyo kitovu cha kampeni hiyo ya kijeshi ya Israel Kamal Abu al-Ruba ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali ni mbaya kwenye eneo hilo.

Amesema matingatinga ya vikosi vya Israel yametifua barabara zote zinazoelekea kambi ya wakimbizi ya Jenin na hospitali ya serikali ya mji huo na kwamba kuna milio ya risasi na mabomu kila baada ya muda mfupi.

Bassam al-Hariri, ni muuguzi kwenye hospitali ya serikali ya mji wa Jenin, "Tumewatibu majeruhi na tumepokea waliokufa. Hivi sasa hakuna majeruhi au mgonjwa anayeweza kufika hapa. Hospitali hii imekuwa kama gereza kwa walio ndani. Hakuna chakula, na vifaa vya matibabu vinaelekea kwisha. Tunaomba Mungu awasaidie wagonjwa na jamaa zao."

Guterres aelezea wasiwasi wake hali ya Jenin huku misaada ya kiutu ikiingia Gaza 

Sehemu ya vifurushi vya misaada ya kiutu inayotolewa kwenye Ukanda wa Gaza. Picha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/Getty Images

Kwa upande wake msemaji wa jeshi la Israel Nadab Shoshani amewaambia waandishi habari kuwa opereshni hiyo inanuwia kuzuia mamia ya mashambulizi ya kigaidi yanayopangwa ndani ya Ukingo wa Magharibi na Israel kwenyewe.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yenyewe imesema uvamizi huo ni sehemu ya mpango wa Israel wa kulitwaa taratibu eneo lote la Ukingo wa Magharibi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amevirai vikosi vya Israel kujizuia na matumizi ya nguvu na ameelezea wasiwasi wake mkubwa na uvamizi huo wa Jenin.

Katika hatua nyingine mamia ya tani za misaada ya kiutu imeendelea kuwasili kwenye Ukanda wa Gaza ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Hapo jana tani 1,670 za chakula zilikuwa zikitayarishwa kuingia Gaza chini ya uratibu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Qatar linaloendesha shughuli zake kutokea Jordan.

Shehena kubwa ya misaada inayojumuisha chakula, mahema na vifaa vya matibabu na vilitazamiwa kuwasili Gaza. Makubaliano ya kusitisha mapigano yaendelekeza malori 600 ya misaada yaruhusiwe kuingia Gaza kila siku ili kusaidia mamia kwa maelfu ya watu walio kwenye hali duni baada ya miezi 15 ya vita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW