"Rushwa inaitafuna China"
8 Novemba 2012Mkutano huo wa wiki nzima na unaotizamiwa kutetua viongozi wapya wa chama na taifa, unahudhuriwa na wajumbe elfu mbili waliyokusanyika katika ukumbi wa Cavernous mjini Beijing, na unafanyika huku kukiwa na machafuko ya kijamii na hasira za umma dhidi ya kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, na pengo linalozidi kupanuka kati ya walicho nacho na wasiyo nacho.
"Kama tutashindwa kushughulikia suala larushwa vizuri, linaweza kkusababisha kuanguka kwa chama na taifa kwa ujumla. Mageuzi ya mifumo ya kisiasa ya chama ni muhimu kama sehemu ya mageuzi ya ujumla ya China. Laazima tuendelee kufanya juhudi za maksudi kugeuza mfumo wa kisiasa, na kupanua demokrasia kwa vitendo," alisema rais Hu.
CPC Kuendelea kutawala kwa muda mrefu
Lakini hakuna anayetarajia demokrasia kamili, na msemaji wa chama cha CPC, Cai Mingzhao alibainisha wazi siku ya Jumatano kuwa utawala wa chama kimoja hauwezi kukiukwa. Chama hicho kimemfukuza kiongozi wake mwanadamizi Bo Xilai na kumtuhumu kwa matumizi mabaya ya ofisi, kuchukua rushwa na makosa mengine katika tukio lililopekelea kuanguka kwa mwanasisa huyo na kusababisha mtikisiko katika chama.
Hu alisema kuwa hawapaswi kuacha maneno yachukue nafasi ya sheria au nguvu ya mtu ichukuwe nafasi hiyo, na kuongeza kuwa hawatakubali kupuuza sheria kwa maslahi binafsi. Wakati wa mkutano huo, Hu atajivua majukumu yake kama kiongozi wa chama na kuyakabidhi kwa mrithi wake, makamu wa rais Xi Jinping. Xi baadae atachukua mamlaka kamili ya kuiongoza China wakati wa mkutano wa mwaka wa bunge mwezi Machi mwaka ujao wa 2013.
Jeshi imara ni muhimu kwa China imara
Zikiwa ni wiki chache tu tangu nchi hiyo ikumbwe na maandamano ya hasira dhidi ya Japan kuhusiana na mzozo wa visiwa, Hu alisema China inapaswa kuimarisha jeshi lake, kulinda maslahi yake ya baharini na kuwa tayari kwa kile alichokiita 'vita vya kienyeji' katika zama hizi za teknolojia ya mawasiliano. Usalama uliimarishwa katika eneo la ukumbi huo na uwanja wa Tiananmen uliyoko jirani, ambao ulishuhudia maandamano ya kudai demokrasia mwaka 1989, yaliyosambaratishwa na jeshi.
Chama cha kikomunisti, kilichokuja madarakani mwaka 1949 kufuatia vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe, kimejikita katika ukuzaji wa uchumi katika miaka ya hivi karibuni na kuwainua mamilioni ya raia wa nchi hiyo kutoka katika dimbwi la umaskini. Hu alisema maendeleo ya China yanapaswa kuwa na urari zaidi, yenye kuratibiwa na endelevu, na kwamba nchi hiyo laazima izidishe jumla ya pato lake la ndani la mwaka 2010 kwa mara mbili ifikapo mwaka 2020.
Lakini wataalamu wa China wanasema bila uongozi mpya kutekeleza mageuzi yaliyokwama, nchi hiyo itakabiliwa na kuzorota kwa uchumi, kuongezeka kwa machafuko, na hata mgogoro unaoweza kutishia uwepo wa chama hicho madarakani.
Wasiwasi juu ya kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi
Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini China ilipungua kwa robo ya saba mfululizo mwezi Julai hadi Septemba, huku serikali ikikosa shabaha zake kwa mara ya kwanza tangu mgogoro wa kiuchumi ulivyofikia kiwango cha juu, lakini taarifa nyingine zinaonyesha ukuaji mdogo wa mwisho wa mwaka.
Watetezi wa mageuzi wanamtaka Xi apunguze upendeleo kwa mashirika ya serikali, kuwezesha wahamiaji wa vijijini kupata makaazi ya kudumu mijini, kurekebisha mfumo wa fedha unaozihamasisha serikali za mitaa kupokonya ardhi, na juu ya yote, kupunguza nguvu za serikali ambazo wanasema zinahatarisha kukwamisha ukuaji na kuchochea manung'niko.
Wakati mkutano huo unaanza, kundi la kutetea haki za binaadamu la Tibet liliripoti kuwa masufii watatu wa Tibet katika jimbo la kaskazini magharibi la Sichuani walijichoma moto kupinga utawala wa China, na kufanya idadi ya Watibet waliyojichoma moto katika miezi 18 kufikia 70.
China imewaita watu hao wanaojichoma kuwa ni magaidi na wahalifu na inawalaumu watibet waliyoko uhamishoni na kiongozi wao Dalai Lama kwa kuwachochea.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman