1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rushwa yaongeza ugumu kwenye mzozo wa corona

28 Januari 2021

Mataifa yenye viwango vya chini vya rushwa yamefanya vizuri katika kuushughulikia mzozo wa virusi vya corona ulimwenguni ikilinganishwa na mataifa yaliyoelemewa na mzigo wa ufisadi.

Schweiz Davos | World Economic Forum | Delia Matilde Ferreira Rubio
Picha: picture-alliance/dpa/A. della Valle

Tuliangazie janga la virusi vya corona ulimwenguni:

Tukianzia ripoti ya kitafiti iliyochapishwa hii leo inayoonyesha kwamba mataifa yaliyo na kiwango cha chini cha rushwa yamekuwa katika nafasi nzuri ya kupambana na changamoto za kiafya na kiuchumi zinazoletwa na janga la virusi vya corona.

Tukiitupia jicho ripoti hiyo iliyochapishwa na taasisi ya kimataifa ya kupambana na ufisadi Alhamisi hii, mataifa yenye kiwango kidogo cha rushwa yamefanikiwa pakubwa katika kukabiliana na athari za kiuchumi na kiafya, zinazosababishwa na janga la virusi vya corona. Ripoti hii inachapishwa mwaka mmoja baada ya taasisi hiyo kufuatilia kwa karibu athari hizo.

Kulingana na taasisi hiyo ya Transparency International kwenye ripoti hiyo inayoangazia dhana ya ufisadi ulimwenguni kwa mwaka 2020, ikitupia jicho zaidi dhana ya rushwa kwenye sekta ya umma, ikiwahoji wataalamu na wafanyabiashara na kuhitimisha kwamba mataifa yaliyofanya vizuri yaliwekeza zaidi kwenye sekta ya afya lakini pia walijizuia kukiuka misingi ya kidemokrasia.

Mkuu wa taasisi hiyo yenye makao yake mjini Berlin Delia Ferreira Rubio amenukuliwa akisema COVID-19 sio tu ni mzozo wa kiafya na uchumi bali pia ni mzozo wa ufisadi na ambao jamii inashindwa kuudhibiti, na kuongeza kuna mahusiano makubwa kati ya ufisadi na namna ya kulishughulikia janga la COVID-19.

Ulaya.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier amesema uchumi wa Ujerumani utakua kwa kiwango cha chini.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance/dpa

Barani Ulaya, nchini Ujerumani waziri wa masuala ya uchumi Peter Altmaier amezungumzia suala la ukuaji wa uchumi ikilinganishwa na matarajio ya awali, akisema uchumi wa taifa hilo utakua kwa kasi ndogo kutokana na athari za janga la corona, ingawa ameahidi kurejea katika hali ya kawaida baada ya muda mfupi.

"Tunatarajia kuerejea kwenye kiwango kilichoshuhudiwa kabla ya mripuko wa corona, kuanzia nusu ya pili ya mwaka ujao. Hata hivyo tunatakiwa kuanza kufikiria kuhusu namna maendeleo yatakavyosonga mbele na ndio maana ninataka kusema kwa nafsi yangu kama waziri kwamba ninasimamia maoni kwamba ongezeko la kodi halitafaa katika kipindi hiki cha mzozo." alisema Altimaier.

Huko mjini The Hague nchini Uholanzi, jeshi la polisi limesema kumekuwepo na utulivu kwa usiku wa nne baada ya maandamano ya kupinga vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona. Hata hivyo jeshi hilo linawashikilia watu 131 kwa makosa ya uharibifu na uchochezi.

Tizama Zaidi: 

Umetimia mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha corona kuthibitishwa Ujerumani

01:33

This browser does not support the video element.

Asia.

Tukielekea Barani Asia, nchini Japan, rais wa kamati ya michuano ya Olimpiki Thomas Bach amesisitiza kwamba wadau wote wamejitoa kikamilifu kufanya mashindano hayo ya majira ya joto, baada ya kuahirishwa kwa mwaka mmoja. Bach amepuuza minong'ono kuhusu kuahirishwa tena kwa michuano hiyo, lakini swali kubwa bado linasalia ni kwa namna gani na iwapo michuano hiyo itafanyika katika mazingira ya sasa na hasa kwa kuwa kiwango cha maambukizi nchini Japan bado kiko juu.

Na wakati hayo yakiendelea, kamati ya kitaifa ya Olimpiki nchini Israel imesema itahakikisha inawachanja washiriki wake wote watakaokwenda kwenye michuano hiyo ifikapo mwezi Mei. Bado kuna mjadala kuhusu iwapo washiriki wanatakiwa kupewa kipaumbele cha chanjo.

Afrika Mashariki.

Huko Afrika Mashariki, nchini Tanzania rais John Magufuli amesema jana kwamba taifa hilo halitahitaji kufunga shughuli ili kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi kwa kuwa linalindwa na Mungu, huku akiendelea kupigia debe tiba ya kujifukiza akisema ni bora zaidi kuliko chanjo hatari zinazotoka Ulaya.

Kauli yake hiyo inakinzana na ushauri wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO lakini pia wanasanyansi. Tanzania ilikwishaachana na hatua ya kuvaa barakoa ama kujitenga na iliacha kutoa taarifa za maambukizi tangu katikati ya mwaka 2020, iliporipoti visa 509 na vifo 21 vilivyotokana na COVID-19.

Mashirika: DPAE/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW