1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine: Russia yafanya mashambulizi ya "kinyama" Krismas

26 Desemba 2024

Russia ilishambulia sekta ya nishati siku ya Krismasi, ikiwacha maelfu bila umeme, mtu mmoja akiuawa na sita kujeruhiwa, huku Zelenskiy akilaani mashambulizi hayo kama "yasiyo ya kibinadamu."

Ukraine Dnipropetrovsk 2024 | Wazima moto wakikabiliana na athari za shambulio la makombora ya Urusi.
Wazima moto wakikabiliana na athari za shambulio la makombora ya Urusi katika mkoa wa Dnipropetrovsk, Ukraine, Desemba 25, 2025.Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Russia ilishambulia mfumo wa nishati wa Ukraine na baadhi ya miji siku ya Jumatano kwa makombora ya masafa marefu na makombora ya balistiki pamoja na droni, katika kile ambacho Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alikilaani kama shambulizi "lisilo la kibinadamu" siku ya Krismasi. 

Karibu miaka mitatu tangu vita kuanza, mashambulizi hayo yaliwajeruhi watu wasiopungua sita katika mji wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv na kumuua mmoja katika mkoa wa Dnipropetrovsk, kwa mujibu wa magavana wa maeneo hayo. 

Rais wa Marekani Joe Biden alilaani shambulio hilo kuwa "lenye kushtusha" na kusema ameiagiza Wizara ya Ulinzi ya Marekani kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine. 

Nusu milioni ya watu katika mkoa wa Kharkiv walibaki bila joto la majumbani, huku joto likiwa chini ya nyuzi chache za Selsiasi, na mji mkuu Kyiv pamoja na maeneo mengine yakipata umeme wa mgao. 

"Leo, (Rais wa Russia Vladimir) Putin aliamua makusudi kushambulia siku ya Krismasi. Kuna kitu gani cha kikatili zaidi? Zaidi ya makombora 70, yakiwemo ya balistiki, na zaidi ya droni 100 za mashambulizi," alisema Zelenskiy. 

Wizara ya Ulinzi ya Russia ilithibitisha kuwa imefanya "shambulio kubwa" kwenye kile ilichokitaja kuwa miundombinu muhimu ya nishati inayosaidia kazi za "sekta ya kijeshi-viwanda" ya Kyiv. 

Operesheni ya wazima moto baada ya shambulio la droni ya Urusi huko Kharkiv.Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

"Lengo la shambulio limefanikiwa. Vituo vyote vimeharibiwa," ilisema katika taarifa. 

Jeshi la Ukraine limesema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilidungua makombora 59 ya Russia na droni 54 usiku kucha na asubuhi ya Jumatano. 

Biden, ambaye atakabidhi uongozi kwa Donald Trump mwezi ujao, alisema shambulio hilo lililenga "kukata upatikanaji wa joto na umeme kwa watu wa Ukraine wakati wa baridi kali na kuhatarisha usalama wa miundombinu yake." 

Washington imetoa msaada wa dola bilioni 175 kwa Ukraine, ingawa kasi ya msaada huo haijulikani itakuwaje chini ya uongozi wa Trump, ambaye ameahidi kumaliza vita haraka. 

Nchini Moldova, jirani wa magharibi wa Ukraine, Rais mwenye mwelekeo wa Ulaya, Maia Sandu, alisema kombora moja la Russia lilivuka anga ya nchi yake wakati wa shambulio hilo. 

"Wakati nchi zetu zinaadhimisha Krismasi, Kremlin imechagua njia ya uharibifu, ikishambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine na kukiuka anga ya Moldova," Sandu aliandika kwenye mitandao ya kijamii. 

Rais wa Moldova Maia Sandu amesema kombora moja la Urusi lilipita katika anga la nchi yake.Picha: Elena Covalenco/DW

Moldova imekuwa na visa kadhaa vya vipande vya droni kuanguka katika ardhi yake na makombora kupita angani mwake. 

Waukraine waliadhimisha Krismasi yao ya pili Jumatano kwa mujibu wa kalenda mpya, hatua nyingine ya kufuta ushawishi wa Russia. 

Soma pia: Putin afanya mazungumzo ya nadra na Waziri Mkuu wa Slovakia

Wengi wa Waukraine ni Wakristo wa Orthodox, na Kanisa Huru la Orthodox la Ukraine, lililoanzishwa mwaka 2018, lilikubali mwaka 2023 kuhama kutoka kalenda ya Julian inayotumiwa na Russia, ambapo Krismasi huadhimishwa Januari 7. 

Russia imeongeza mashambulizi yake kwenye sekta ya nishati ya Ukraine tangu msimu wa machipuko mwaka huu, ikiharibu karibu nusu ya uwezo wake wa kuzalisha nishati na kusababisha mgao wa umeme wa muda mrefu. 

SIku 1,000 za vita vya Ukraine

01:44

This browser does not support the video element.

'Russia inatumia baridi kama silaha'

Jeshi la anga la Ukraine lilisema Kharkiv ilishambuliwa na makombora ya balistiki. Gavana wa mkoa wa Kharkiv, Oleh Syniehubov, alisema kupitia Telegram kuwa kulikuwa na uharibifu wa miundombinu ya kiraia isiyo ya makazi, bila kutoa maelezo zaidi. 

Gavana wa Dnipropetrovsk, Serhiy Lysak, alisema kifo katika mkoa huo kilitokea wakati wa shambulio la miundombinu ya nishati ya mkoa huo. 

"Tangu asubuhi, jeshi la Russia limekuwa likishambulia kwa nguvu mkoa wa Dnipro. Linajaribu kuharibu mfumo wa nishati wa mkoa huo," alisema. 

Waziri wa Nishati wa Ukraine, German Galushchenko, alisema kupitia Facebook kuwa Russia inashambulia sekta ya nishati kwa kiwango kikubwa na kwamba mgao wa umeme umewekwa. 

Kampuni kubwa zaidi ya nishati binafsi nchini Ukraine, DTEK, ilisema vituo vyake vya kuzalisha nishati vilishambuliwa, na vifaa vya nishati viliharibiwa vibaya, katika shambulio la 13 la mwaka huu kwenye sekta ya nishati. 

Mashambulizi ya Urusi yamelenga zaidi miundombinu ya nishati ya Ukraine na kupelekea mgao wa mara kwa mara wa umeme.Picha: UKRAINIAN EMERGENCY SERVICE/HANDOUT/AFP

"Tunatoa wito kwa kila mshirika wa Ukraine kumaliza ugaidi huu unaodhaminiwa na serikali sasa kwa kuvipa vikosi vyetu vya mifumo ya ulinzi wa anga vinyoihitaji kulinda miundombinu muhimu ya nishati," Mkurugenzi Mtendaji wa DTEK, Maxim Timchenko, alisema katika taarifa. 

Soma pia: Rais Zelensky aomba washirika wa Ulaya kuwasaidia kwa umoja

"Zawadi ya Krismasi ya Russia kwa Ukraine: zaidi ya makombora 70 na droni 100, yakilenga familia za Waukraine wanaosherehekea majumbani mwao na miundombinu ya nishati inayowapa joto," alisema Balozi wa Marekani Bridget Brink. 

"Kwa msimu wa tatu wa sikukuu, Russia inatumia baridi kama silaha."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW