Ruto aahidi huduma za serikali kwa Wakenya wote
12 Desemba 2022Zaidi ya Wakenya elfu 20, walifurika kwenye uwanja wa taifa wa Nyayo, jijini Nairobi kuhudhuria siku kuu ya Jamhuri, Kenya inapofikisha miaka 59 tangu ipate hadhi hiyo mwaka 1964, mwaka mmoja baada ya kujinyakulia uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1963.
Rais William Ruto aliyechukua usukani kuongoza hafla hiyo mwezi mmoja tangu aapishwe alikuwa na ahadi chungu nzima kwa wakenya wanaokabiliwa na athari za kupanda kwa gharama ya maisha.
Ruto amewataka wakenya kuwa na subira serikali yake inapoweka mikakati ya kuimarisha hali. Aliangazia suala la ajira kwa vijana, akiahidi serikali yake itawasaidia wakenya wote wenye mawazo ya uvumbuzi kwa sababu ya kuboresha uchumi. Ruto alisma kuwa kwa sasa ni asilimia 15 tu ya huduma za serikali zinazotolewa kwa njia ya dijitali.
Uadilifu wa polisi ?
Kwenye hotuba yake kwa taifa iliyochukua zaidi ya saa nzima na kupeperushwa na vyombo vyote vya habari nchini, Rais alikisifu kikosi cha polisi kwa uadilifu wake tangu achukue hatamu za uongozi na kuahidi kukiimarisha kikosi hicho.
Kwa muda mrefu mazingira ya utendaji wa polisi yamekuwa duni , wakilalamikia mishahara midogo, ukosefu wa makazi bora, hali ambayo imewafanya wengi kujihusisha na vitendo vya ufisadi kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari
Wakati wa kampeini ya kuomba kura, Ruto na mgombea mwenza Rigathi Gachagua, waliahidi kuwa serikali ya Kenya Kwanza itarejesha hadhi ya wafanyikazi wa umma iwapo wangeshinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi wa nane. Naibu Rais Gachagua ambaye amekuwa akiukosoa upinzani mara kwa mara amesema, uongozi wa Kenya Kwanza utawakomboa wakenya.
Sherehe ya leo imehudhuriwa na waakilishi kutoka kampuni za Facebook, Youtube, Google, Microsoft na Multichoise, ishara ya kutia chachu bango la kauli ya Tehama na Uvumbuzi.