Rais Ruto aahidi kuimarisha ushirikiano wa Kenya na Tanzania
10 Oktoba 2022Masuala yanayohusu biashara ndiyo yaliyonekana kujitokeza zaidi wakati viongozi hao walipokuwa na mazungunzo ya faragha na baadaye kuungana na watendaji wao ambao wamepewa majukumu ya kuyakamilisha masuala yote yatakayoimarisha ushirikiano mwema kwa mataifa hayo mawili yaliyo waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Uganda.
Viongozi hao wametaka vikwazo vya kibiashara vinavyoendelea kutatiza pande hizo mbili viondolewe, na Rais Ruto anasema angependa kuona hayo yanakamilika ndani ya mwaka huu.
Kazi ya pamoja iliyoasisiwa kati ya Rais Samia na Rais Uhuru Kenyatta aliyemaliza muda wake ilisaidia kufungua ukurasa mpya wa kibiashara hali iliyoshuhudia vikwazo 68, vikitafutiwa majawabu na kusalia vikwazo 14.
Kwa maana hiyo Rais Ruto amesema kazi iliyoasisiwa na viongozi hao itaendelea kuwa sehemu ya vipaumbele vyake na amehaidi kuvimaliza vikwazo hivyo ifikapo Disemba mwaka huu.
Kauli zinazoshabiana
Mbali na masuala ya ukuzaji biashara na ujirani mwema, viongozi hao wamejadiliano pia kuhusu masuala yahusuyo ulinzi wa mipaka wakilenga kukabiliana na vitendo vya kihalifu ikiwemo kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
Rais Samia amesema Tanzania na Kenya zitaendelea kuwa na kauli zinazoshabiana katika majukuwaa ya kimataifa kama vile ndani ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Rais Ruto aliyeshinda uchaguzi wa Agosti 9 aliwasili nchini jana jioni kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili akiwa ameambatana na maafisa wake. Inakuwa ni ziara yake ya kwanza nchini Tanzania na aliyeofanya kwa kipindi cha muda mfupi tangu aiingie madarakani Septemba 13. Baadaye leo ataandaliwa dhifa ya kitaifa kabla ya kurejea Nairobi.