1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aanza ziara pwani ya Kenya

27 Julai 2023

Rais William Ruto ameanza ziara yake ya siku tano katika eneo la pwani ya Kenya, akitembelea Kaunti za Lamu na Tana River ambako amezindua miradi mbalimbali inayotarajiwa kuinua uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Der keniansiche Präsident William Ruto in Südafrika
Picha: Ihsaan Haffejee/AA/picture alliance

Ruto alikaribishwa kwa vifijo na nderemo katika Kaunti ya Lamu mapema siku ya Alkhamis (Julai 27), ambako alitarajiwa kuzinduwa miradi inayohusiana na uchumi wa baharini pamoja na kuifungua ofisi ya makamishna wa kaunti hiyo.

Majira ya mchana, Rais Ruto alivuuka hadi Kaunti ya Tana River ambako pia alizinduwa mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji katika mashamba ya mpunga ya Tarda. 

Soma zaidi: Ruto: Niko tayari kukutana na Odinga wakati wowote

Mradi wa Tarda unaotarajiwa kutoa ajira zaidi ya 8,000 kwa wakaazi wa eneo hilo, unakusudiwa kuimarisha kilimo cha mpunga na kupunguza uagizaji mchele kutoka nchi za nje kwa asilimia 35 kulingana na ajenda ya serikali ya Ruto juu ya upatikanaji wa chakula.

Ruto akwepa kuzungumzia siasa

Ruto, ambaye yupo kwenye mtihani wa kisiasa kutokana na maandamano ya umma yanayoandaliwa na uongozi wa upinzani, kwa kiasi kikubwa alionekana kuepuka kuzungumzia zaidi hali ya kisiasa.

Rais William Ruto (kushoto) na makamu wake, Rigathi Gachagua.Picha: Simon Maina/AFP

Matukio ya karibuni ya maandamano yenye ghasia yaliyoitishwa na upinzani kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha, ambapo watu kadhaa waliuawa kwa kupigwa risasi huku mali zikiharibiwa. 

Soma zaidi: Kenya yabadili hukumu ya kifo kuwa kifungo cha maisha

Wachambuzi wanahisi kuwa kuna uwezekano wa kuwepo mazungumzo kati ya Ruto na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, baada ya wote wawili kuonyesha kuwa tayari kukutana ila kwa masharti.

Wapinzani wamesema watatangaza hatua zinazofuata baada ya kusitisha kwa muda maandamano yao yaliyokuwa yamepangwa kuendelea wiki hii. 

Mkutano na jamii ya Wapemba

Siku ya Ijumaa (Julai 27), Rais Ruto anatarajiwa kuzuru jamii ya Wapemba katika Kaunti ya Kilifi kwa ajili ya kuwapa vitambulisho vya kitaifa. Hii ni baada ya jamii hiyo kutambuliwa na serikali ya Kenya kupitia tangazo rasmi la rais la Januari 2023.

Meli ikiwa imetia nanga kwenye bandari ya Mombasa.Picha: AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali, Hussein Mohammed, amesema siku ya Jumamosi, kiongozi huyo wa Kenya atakuwa mjini Mombasa kuhudhuria mikutano mbalimbali ikiwemo kukutana na wadau wa bandari ya Mombasa ambako pia ataizindua rasmi meli ya kivita ya KNS Shupavu.

Soma zaidi: Kenya yahitimisha siku ya tatu ya maandamano

Kwenye ziara hii, ofisi ya Rais Ruto imesema vikundi mbalimbali vya uvuvi na miradi mingine kutoka Lamu, Kilifi, Mombasa na Kwale vitapokea zaidi ya shilingi milioni 500 (sawa na dola za Kimarekani milioni 3.5) kwa ajili ya kuendeleza miradi yao.

Imeandaliwa na Halima Gongo/DW Mombasa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW