Ruto na mlima wa kudhibiti maandamano, kuwashawishi Gen Z
9 Julai 2025
Wimbi jipya la maandamano linaloongozwa na kizazi cha vijana maarufu kama Gen Z nchini Kenya limeendelea kumweka Rais William Ruto katika hali ya wasiwasi, huku kauli maarufu ya waandamanaji "Ruto wantam” – ikiwa na maana ya kutaka rais huyo aongoze kwa muhula mmoja tu – ikisambaa mitaani.
Ruto alichaguliwa karibu miaka mitatu iliyopita kwa ahadi ya kuwalinda maskini na kukomesha ukatili wa polisi, lakini hali ngumu ya kiuchumi, madai ya rushwa na ukandamizaji wa raia vinaendelea kuchochea hasira za wananchi. Kwa sasa, kiongozi huyo anahisi ukali wa vijana waliotayari kuingia barabarani kupaza sauti zao.
Wachambuzi wanasema kuwa endapo Ruto anataka kupata muhula wa pili mwaka 2027, atalazimika kutimiza ahadi zake za kiuchumi na kuacha msimamo mkali. Badala yake, atahitaji kujenga maelewano zaidi na kizazi cha sasa cha vijana walioelimika na wanaotumia mitandao ya kijamii kwa ustadi mkubwa kushinikiza mabadiliko.
"Shida za kiuchumi na madai ya ukatili wa polisi vinaweza kuwa vizuizi vikubwa kwa matarajio ya Ruto ya kuchaguliwa tena,” alisema Mucahid Durmaz, mchambuzi wa masuala ya Afrika katika shirika la Verisk Maplecroft.
Katika maandamano ya hivi karibuni yaliyofanyika Jumatatu, watu 31 walithibitishwa kuuawa kote nchini, kulingana na ripoti ya shirika la haki za binadamu linaloendeshwa na serikali. Polisi walitumia risasi, gesi ya kutoa machozi na mizinga ya maji kuwatawanya waandamanaji.
Gen Z wapaza sauti: "Tunataka Rais atusikie”
"Nchi yetu haijatujali. Hatuwezi kulisha familia zetu. Tuko barabarani kuzuia kupanda kwa bei, kupinga utekaji nyara unaofanywa na polisi, na kutetea taifa letu,” alisema Festus Muiruri, kijana mwenye umri wa miaka 22 aliyekuwa akishiriki maandamano mjini Nairobi.
Lakini serikali ya Ruto imekuwa na mwitikio wa taratibu mno kwa matakwa ya umma. Mwaka jana, ilibidi afute mapendekezo ya kuongeza kodi baada ya waandamanaji kuvamia bunge kwa mara ya kwanza kabisa – tukio lililorushwa moja kwa moja kwenye runinga duniani kote.
Waziri wa mambo ya ndani, Kipchumba Murkomen, aliwataja waandamanaji wa Juni kama "magaidi” waliotaka kufanya "jaribio la mapinduzi.”
Tofauti na marais waliomtangulia, Ruto anakabiliwa na kizazi kipya cha vijana waliokomaa kisiasa, wanaotumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la harakati bila kutegemea wanasiasa wa upinzani.
Vijana hawa wa Gen Z, waliopata elimu ya bure tangu miaka ya 2000, hawana kumbukumbu ya utawala wa kiimla. Wengi wao walizaliwa baada ya Kenya kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Ripoti ya Afrobarometer inaonyesha kuwa kila mwaka, vijana takribani 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira. Ingawa wengi wao wameelimika kuliko wazazi wao, bado hawana ajira, hali inayozidisha hali ya kukata tamaa.
Kifo cha bloga chazua moto
Hasira dhidi ya serikali ziliongezeka mwezi uliopita kufuatia kifo cha blogger Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi. Tarehe 25 Juni, takribani watu 19 walikufa kwenye maandamano yaliyohusiana na kifo hicho.
Matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji yameanza kuwatisha wawekezaji katika uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Utafiti wa Stanbic Bank Kenya ulionesha kuwa matarajio ya wafanyabiashara yaliporomoka mwezi Mei hadi kiwango cha pili cha chini kabisa kuwahi kurekodiwa.
"Maandamano ya mara kwa mara na kufungwa kwa shughuli yataendelea kuathiri imani ya wawekezaji na kuzuia ukuaji wa kiuchumi, hasa kama serikali itaendelea kutumia nguvu badala ya mazungumzo,” alisema Jervin Naidoo wa shirika la Oxford Economics.
Licha ya hali hii, Bunge kubwa la chama tawala linalodhibitiwa na Ruto linamkinga dhidi ya tishio lolote la kung'olewa madarakani kwa sasa.
Aidha,upinzani umedhoofika na bado haujampata mgombea mwenye mvuto kwa uchaguzi wa 2027. Kwa kumuingiza Raila Odinga katika mazungumzo ya kitaifa mwaka jana, Ruto alifanikiwa kumdhibiti mpinzani wake mkuu.
Uchaguzi wa 2027: Ruto atakwepa "Wantam"?
Kwa mujibu wa shirika la Control Risks, Ruto atatumaini kuwa ongezeko la matumizi ya kijamii, mipango ya kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, pamoja na kuimarika kwa uchumi na kushuka kwa mfumuko wa bei, vitasaidia kubadili taswira yake.
Hata hivyo, wachambuzi kama Javas Bigambo wanaonya kuwa hayo hayatoshi kumuepusha na hatima ya kuwa rais wa kipindi kimoja tu.
"Kuna mtazamo miongoni mwa vijana kuwa serikali ni kipofu, kiziwi na bubu. Hali hii ikiachwa bila kurekebishwa, itaongeza mgawanyiko kati ya serikali na wananchi,” alisema Bigambo.
"Ni muhimu hatua zichukuliwe haraka kupunguza mgawanyiko huo.”
Wakati huo huo, mashirika ya haki za binadamu yameripoti kuwa watu 107 walijeruhiwa, na zaidi ya 500 kukamatwa katika maandamano ya Jumatatu – ambayo ndiyo yaliyokuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo kwa siku moja tangu maandamano kuanza mapema mwaka huu.
Hata hivyo, Rais Ruto hajatoa tamko lolote kuhusiana na maandamano hayo au vifo vilivyotokea.
Historia ya Saba Saba yajirudia
Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani, alisema kuwa mkuu wake Volker Türk "anarudia wito wa utulivu, heshima kwa uhuru wa kujieleza, kuandamana na kushiriki.”
Maandamano ya Jumatatu yaliyoratibiwa kuadhimisha miaka 35 ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba, yalizuiwa na vizuizi vya polisi vilivyowekwa katikati ya jiji la Nairobi. Siku hiyo, tarehe 7 Julai, ni kumbukumbu ya maandamano ya mwaka 1990 yaliyolazimisha utawala wa Daniel Arap Moi – aliyekuwa mlezi wa kisiasa wa Ruto – kuachana na mfumo wa chama kimoja.
Maandamano ya mwaka huu yaliibuliwa na kifo cha blogger mikononi mwa polisi mwezi uliopita. Polisi pia walimpiga risasi mtu kwa karibu wakati wa maandamano ya Juni 17. Tarehe 25 Juni, maelfu ya vijana waliandamana kote nchini.
Kwa ujumla, watu 50 wamepoteza maisha kutokana na maandamano katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wa Kenya (NCIC), chombo cha serikali kilicho chini ya mamlaka ya rais, iliwasihi wanasiasa wasitumie maandamano kama fursa ya kuchochea chuki za kikabila, na pia ilikosoa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.
Miaka 35 baada ya Saba Saba, sauti za vijana hazizuiliki
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen aliwaamuru polisi "kupiga risasi moja kwa moja" kwa yeyote anayekaribia vituo vya polisi wakati wa maandamano, baada ya baadhi ya vituo hivyo kuchomwa moto.
Hasira ya wananchi pia imechochewa na juhudi za serikali kulazimisha wananchi kulipa kodi zaidi ili kufidia madeni makubwa ya taifa. Mwaka jana, maelfu ya vijana waliandamana kupinga kodi na kuvamia bunge, jambo lililomlazimisha Ruto kuahidi kupunguza matumizi ya serikali.
Wakati baadhi ya watu walitumia machafuko hayo kufanya uhalifu, wafanyabiashara wengine wamelalamika kuhusu hasara kubwa ya bidhaa.
"Tuliingiliwa dukani, na ukweli ni kwamba tumepoteza vitu vingi sana. Tumepoteza pesa taslimu, simu nyingi – ni hasara kubwa,” alisema Nancy Gicharu, mfanyabiashara wa simu za mkononi.
Katika hali inayoonekana kurudia historia ya vuguvugu la demokrasia la Saba Saba, vijana wa kizazi cha sasa wameonyesha kuwa wako tayari kusimama kidete kudai haki zao, hata mbele ya risasi na mabomu ya machozi.
Iwapo Rais William Ruto atakosa kusikia kilio chao na kushughulikia kero zao, historia huenda ikajirudia – kwa mara nyingine kupitia sanduku la kura au kwa maandamano yasiyoisha mitaani.