1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aongoza kutoa heshima za mwisho kwa Raila

Shisia Wasilwa
17 Oktoba 2025

Rais William Ruto ameliongoza taifa la Kenya kumpa heshima za mwisho hayati Raila Amollo Odinga katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi kabla ya maziko nyumbani kwake Bondo, jimbo la Siaya siku ya Jumapili.

2025 Kenya Nairobi | Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga afariki akiwa na umri wa miaka 80
Maafisa wakiwa wanasukuma jeneza la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, aliyefariki alipokuwa akitibiwa nchini India, kwa ajili ya ibada ya mazishi katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi, Kenya Oktoba 17, 2025.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Rais William Ruto alimtaja kiongozi huyo mkongwe kama mzalendo na mwanasiasa shupavu ambaye maisha na urithi wake vilizidi mipaka ya siasa aliyeweka kando maslahi yake binafsi kwa manufaa ya nchi nzima.

Akihutubia maelfu ya waombolezaji, wakiwemo marais wa Afrika, viongozi wa kimataifa, na Wakenya kutoka pembe zote za nchi, Rais Ruto alitafakari safari yake ndefu ya kisiasa pamoja na Raila akimtaja kuwa mwalimu, mshindani mwenye nguvu na mtu aliyetoa mchango usiosahaulika katika ujenzi wa demokrasia ya Kenya. Alimpongeza Raila kwa kuisaidia serikali kuwadhibiti vijana wa GenZ walipolivamia bunge la taifa mwaka uliopita wakitaka ang'atuke madarakani kutokana na mswada tata wa fedha.

Kutoka kushoto, Rais wa Kenya William Ruto na mkewe Rachael, Naibu Rais Kithure Kindiki na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta wanahudhuria mazishi ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi, Kenya, Ijumaa, Oktoba 17, 2025.Picha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

"Historia itamhukumu kwa haki na unyenyekevu kwa sababu wakati taifa lilimhitaji kukiuka ubinafsi, alifanya hivyo kwa kujitolea, wakati taifa lilipomhitaji kuwa sauti ya busara alifanya hivyo kwa ujasiri na wakati alipohitajika kuwa mpatanishi alifanya hivyo.”

Kenyatta: Raila alikuwa mtetezi wa haki

Kwa upande wake Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta alimtaja marehemu Raila Odinga kuwa mtetezi wa haki za wanyonge, akiwahimiza Wakenya kuendelea kupigania haki na usawa alizopigania marehemu. "Leo hii, tukiwa tunaaga baba yetu Raila Amollo Odinga naomba tuape ya kwamba hatutakubali kama Wakenya, haki za kibinadamu, demokrasia na mambo yale yote Raila alitetea, yarudi nyuma.”

Upande wa upinzani umekosoa hatua ya kutotambuliwa kwenye hafla hiyo. Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema "Inasikitisha sana, haya ni mazishi ya kitaifa, wangelitambua upinzani, kusema jambo, ndivyo Raila Odinga angependa ifanyike.”

Mwanasiasa mkongwe nchini Kenya Raila Odinga (katikati) akiwahutubia wafuasi wake baada ya kutia saini rasmi mkataba wa ushirikiano wa kisiasa na Rais William Ruto (hayupo pichani) katika nia ya kuimarisha urais wake baada ya miezi kadhaa ya machafuko, jijini Nairobi mnamo Machi 7, 2025.Picha: Simon Maina/AFP

Wageni wa kimataifa wahudhuria

Miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia Hassan Sheikh Mohamud Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango, Rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Vincent Biruta, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Rwanda, aliyemwakilisha Rais Paul Kagame, miongoni mwa wengine.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi