1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto ashutumiwa kuanza njia za kukataa matokeo ya uchaguzi

3 Machi 2022

Kampeni zimeshika kasi ikiwa imesalia miezi 5 kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya. Wapinzani wa naibu wa rais William Ruto sasa wanadai anachelea kushindwa na ameanza harakati za kuyakataa matokeo ya uchaguzi wa Agosti.

Kenia Eldoret - Deputy President William Ruto
Picha: Reuters/T. Mukoya

Muda mfupi baada ya naibu wa Rais William Ruto kutoa hotuba yake Baltimore, Marekani, wapinzani wake wamekuja juu kumkosoa kwa kauli zake kuwa demokrasia iko hatarini na inaandaliwa njama ya kuiba kura.

Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha Orange Democratic, ODM kilicho mshiriika mkuu wa Azimio la Umoja,John Mbadi anasisitiza kuwa kauli hizo zinashangaza.

Dr William Ruto anafanya ziara ya siku 12 ya Uingereza, Marekani na Qatar. Wakati huohuo, chama cha United Democratic Alliance, UDA, Cha naibu wa rais kimepata pigo jipya na kuandamwa na misukosuko. Saa chache zilizopita naibu katibu mwenezi wa UDA,Wanjala Iyaya amejiuzulu na kujiunga na Azimio la Umoja kupitia chama cha DAP-K.

Kulingana na maelezo yake kwenye mtandao wa Twitter, Wanjala Iyaya anapania kugombea ubunge wa kiti cha Webuye Mashariki. Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa wiki hii mweka hazina wa UDA naye pia alikihama chama na kujiunga na Jubilee iliyo mshirika mkuu wa Azimio la Umoja.

Kalonzo atakiwa kufikia muafaka na Odinga

Kiongozi wa ODM Raila OdingaPicha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Yote hayo yakiendelea,kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka, amejikuta kwenye njia panda baada ya wenzake kumtaka atangaze msimamo wake. Kwenye taarifa yao ya pamoja,wadau muhimu wa muungano wa One Kenya Alliance, OKA, wamemtaka Kalonzo Musyoka kufikia mwafaka na kiongozi wa ODM Raila Odinga pasina Masharti.

Kiongozi wa NARC Charity Ngilu na mwenzake wa DAP-K Wafula Wamunyinyi wanasisitiza kuwa madai ya Kalonzo haya msingi. Kauli hizo zinaungwa mkono na gavana wa Makueni Kivutha Kibwana.

Ifahamike kuwa Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni ni mmoja ya mashahidi 4 waliohusika na utunzi wa hati muhimu iliyounda muungano wa NASA uliokufa baada ya uchaguzi wa 2017. Kauli hizo zinaungwa mkono na seneta wa zamani wa kaunti ya Machakos Johnstone Muthama anayetaka kuwania ugavana.

Kwa upande wake, muungano wa Azimio la Umoja umeweka bayana kuwa uko tayari na makini kufanya kazi na kila chama kinachojiunga kivyake ili wawe na sauti kubwa zaidi.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya