1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto atetea rikodi ya uongozi wake wa miaka miwili

16 Septemba 2024

Rais William Ruto wa Kenya ametetea rikodi yake ya miaka miwili madarakani akisema hakuna serikali ya nchi hiyo iliyowahi kuweka mikakati madhubuti ya kuiendeleza Kenya kuliko ile anayoiongoza.

Rais William Ruto| Kenya
Rais William Ruto wa Kenya akizungumza na DW mjini Berlin. Picha: Thomas Kulik/DW

Rais Ruto ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiswahili ya DW yalifanyika mjini Berlin wakati alipofanya ziara ya siku mbili nchini Ujerumani wiki iliyopita. 

Mahojiano maalumu na Rais William Ruto wa Kenya

12:24

This browser does not support the video element.

Ruto alikuwa mjini Berlin kushiriki Tamasha la Wananchi wa Ujerumani ´BürgerFest´ ambalo huandaliwa kila mwaka na Ofisi ya Rais wa Ujerumani, pamoja na kutia saini mkataba utaowezesha maelfu ya Wakenya wenye ujuzi kupata nafasi za kazi nchini Ujerumani.

Akizungumzia malalamiko ya umma juu ya gharama kubwa za maisha na ukosefu wa ajira, Ruto amesema rikodi ya serikali yake haina mpinzani, akijinadi kwamba tangu alipoingia madarakani ameweka mikakati ya makusudi ya kushughulikia changamoto zinazolikabili taifa hilo la Afrika Mashariki.

"Hakuna serikali nyingine iliyowahi kuwa na mpango kama niliokuwa nao mimi. Wa kwanza; mpango wa ujenzi wa makaazi ya gharama nafuu tayari umetengeneza nafasi za ajira 160,000 ... nafasi za kazi zitokanazo na teknolojia ya dijitali ni 140,000," amesema Rais Ruto na kuorodhesha mipango mengine kadhaa anayosisitiza inasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini mwake.

Ruto: Mkataba na Ujerumani ni fursa nyingine ya ajira 

Rais Ruto vilevile ameutetea mkataba aliuotia saini Jumamosi iliyopita na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani akisema utaongeza nafasi za kazi kwa vijana wa Kenya.

Kulingana na kiongozi huyo, mkataba huo utawawezesha wafanyakazi wenye ujuzi mkubwa na wa kati kupata nafasi za ajira nchini Ujerumani. Amezitaji baadhi ya kada zitakazonufaika kuwa ni pamoja na sekta ya afya, elimu na fani za uhandisi na ufundi.

Rais William Ruto wa Kenya (kushoto) alipokutana na Kansela Olaf Scholz mjini Berlin hivi karibuni.Picha: Liesa Johannssen/REUTERS

Akijibu hoja za baadhi ya wanasiasa na vijana wa Kenya wanaoukosoa mpango huo, Rais Ruto amesema, "Hakuna kijana Mkenya ambaye atalazimishwa kwenda mahala popote. Wale ambao tutawasaidia kupata nafasi ya ajira Kenya, hilo litakuwa chaguo letu la kwanza, lakini hatutawazuia vijana wa Kenya ambao azma yao ni kufanya kazi nje ya Kenya." 

Baadhi ya wanasiasa na wananchi waliitumia mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma kukosoa uamuzi wa serikali ya Ruto wa kutia saini mkataba huo wakisema jukumu la serikali ni kutengeneza fursa za ajira ndani ya nchi hiyo badala ya kutafuta fursa hizo kwenye mataifa ya kigeni.

Ruto amesema pamoja na juhudi ambazo serikali yake inachukua, itakuwa vigumu kumaliza tatizo la ukosefu wa ajira nchini Kenya na ndiyo maana mikataba kama ule aliotia saini na Ujerumani ni muhimu.

Takwimu za nchi hiyo zinaonesha zaidi ya vijana wenye ujuzi milioni 1 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na uwezo wa uchumi wake.

Takwimu za Taasisi ya Statista ya nchini Ujerumani, zinaonesha ukosefu wa ajira unaongezeka nchini Kenya na utafikia asilimia 7.5 mwaka 2027 kutoka asilimia 6.3 hivi sasa.

Ruto asema hana hofu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027

Kwenye mahojiano na DW, kiongozi huyo wa Kenya pia amegusia masuala mengine kadhaa ikiwemo hali jumla ya kisiasa kwenye nchi hiyo.

Maandamano ya mwezi Juni, 2024 dhidi ya mipango ya bajeti yalikuwa moja ya yale mabaya kabisa kuitisa Kenya katika miaka ya karibuni. Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Itakumbukwa, serikali yake ilikabiliwa na wimbi kubwa la maandamano ya umma mnamo mwezi Juni ya kupinga mipango yake ya kikodi ambayo yalimlazimisha kuondoa bungeni mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2024/2025.

Amesema pamoja na maandamano yale yaliyogeuka wakati fulani kuwa ya vurugu anaamini wananchi wanayo haki ya kueleza hisia zao kwa sababu Kenya ni taifa la kidemokrasia.

Sehemu ya vuguvugu la maandamano hayo -- yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 20 kutokana na makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama -- ilikuwa ni shinikizo la kumtaka Ruto aondoke madarakani.

Shinikizo hilo halikufanikiwa lakini baadhi ya makundi ya vijana yameapa Ruto atakuwa rais wa muhula mmoja na watahakikisha hatorejea madarakani mnamo 2027 muhula wake wa kwanza utakapomalizika.

Alipoulizwa na mwandishi wa DW Rashid Chilumba kuhusu wasiwasi huo, Rais Ruto amesema "Sina wasiwasi wowote kwa sababu kufikia mwaka 2027 (Wakenya) watakuwa wameona matokeo ya mipango niliyo nayo."

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi