1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto awakosoa wabunge kuhusu sera ya ajira nje ya nchi

wakio Mbogo19 Februari 2024

Rais William Ruto amewakosoa wabunge kwa kutelekeza agenda yake ya kutoa nafasi za ajira zikiwemo nafasi kwenye mataifa ya nje na badala yake amewataka kuunga mkono ajenda hiyo inayonuia kupunguza tatizo la ajira.

Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Ihsaan Haffejee/AA/picture alliance

Akiongoza mkutano wa siku nne wa baraza la mawaziri na viongozi wakuu serikalini ambao unafanyika katika mji wa Naivasha kaunti ya Nakuru, Rais Ruto amechukua fursa hiyo kuwarai viongozi kuwajibika na kuiunga mkono serikali kikamilifu.

Rais amelalamika kwamba serikali yake imetangaza nafasi 2,500 za ajira kwa wauguzi katika mataifa ya nje lakini viongozi hawajachukua hatua ya kujaza nafasi hizo.

Amesema kufikia mwezi Juni watakuwa wamekamilisha mikakati na kutangaza nafasi zingine laki 250,000 za ajira katika taifa la Ujerumani.

"Sasa wewe wakati unaketi kwa huo mkutano hivi, unasikia Rais anasema kuna nafasi ya wauguzi, wewe hujiulizi, ukitoka hapo kwenye mkutano si unaenda kutafuta mahali hao wauguzi wako?”

Amewakosoa wabunge waliodai kuwa hawakufahamishwa kuwa kuna nafasi za ajira kwa wauguzi katika mataifa ya nje.

"Mnataka tugawane hapa. Niwaulize nani alikatazwa kupeleka 20 au 30? Eti hamjaambiwa? Mnataka kuambiwa na nani? Kwani hamsomi gazeti? Na saa ile mimi naongea mnafikiri mimi naongea hewa?"

Katika mkutano huo, Rais ameutetea mswada wa nyumba za bei nafuu na amewahimiza wabunge waupitishe ili kuhakikisha ametimiza ahadi zake kwa wananchi.

Soma pia:Ruto alaumu watendaji wazembe baada ya mripuko wa gesi

Amewasuta wanaopinga mradi huo akisema kuwa serikali inaweka mikakati ya kuhakikihsa kuwa masuala yaliyoibuliwa mahakamani yametatuliwa.

"Tutatekeleza mpango wa nyumba za bei nafuu. Sitaki kusema tutatekeleza kwa njia yoyote iwezekanavyo, nimesema tutatekeleza."

alisema rais Ruto na kuongeza kuwa nchi zingine zilizoendelea zimefanya mpango huo na zimefanikiwa.

"Sio uvumbuzi mpya. Na hata wanaopinga mpango huu sio kwa sababu ni mpango mbaya, lakini wanaupinga kwa sababu ni sisi tunaoutekeleza.”

Mashaka ya muelekeo wa kisiasa Kenya

Mkutano huo unakuja wakati viongozi kutoka eneo la mlima Kenya wanaonekana kutilia shaka mwelekeo wa kisiasa unaochukuliwa na serikali ya Rais.

Kiongozi wa upinzani Kenya Raila OdingaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Ruto ameonekana kumkumbatia kiongozi wa upinzani Raila Odinga na hata kumpigia debe katika uwaniaji wa kiti cha uwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, AU.

Soma pia:Ufisadi Kenya: Mihimili mitatu ya serikali yapewa siku 30

Hata hivyo naibu Rais Rigathi Gachagua hakusita kuonyesha makali yake dhidi ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye hapo jana aliwashauri viongozi serikalini kuacha kushikilia yaliyopita na badala yake wazingatie kuwahudumia wananchi. Akimjibu, Rigathi amesema ni muhimu kuzingatia yaliyopita ili kuganga yajayo.

"Nilimsikia mtu akisema kwamba haufai kutizama nyuma unapoongoza taifa hili, nataka kukuhimiza uangalie nyuma kwa sababu katika uongozi wako alisema bayana kwamba hakuna Mkenya anapaswa kuachwa nyuma, kwa hiyo ni lazima uendelea kuangalia nyuma kuhakikisha hakuna Mkenya amewachwa nyuma.”

Kongamano hilo la pili la viongozi wakuu serikalini linanuia kutathmini utendakazi wa serikali ya Kenya. Baadhi ya masuala yanayozingatiwa na serikali hii ni mpango wa afya kwa wote, bima ya afya ya kitaifa, ukuaji wa uchumi na kubuni nafasi zaidi za ajira.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW