1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto: Kutoka mpwaguzi hadi rais aliechaguliwa Kenya

15 Agosti 2022

William Samoei Arap Ruto, ni miongoni mwa watu ambao ni matajiri sana nchini Kenya, aliyeanzia chini kabisa kama muuza kuku, na hadi leo anapenda kujionesha kama mtetezi wa maskini na wanyonge.

Kenia Präsident William Ruto
Picha: picture-alliance/Photoshot/P. Siwei

Baba wa watoto sita, Ruto mwenye umri wa miaka 55 na ambaye hanywi aina yoyote ya kileo, hachelei kujieleza kuwa Mkristo aliyeokolewa. Mara nyingi hotuba yake haitakamilika bila ya kumshukuru au kumsifu Mungu au kukariri fungu kutoka katika Bibilia.

Baada ya kumaliza masomo, shahada ya sayansi ya mundo wa mimea yaani, Botania, alitia guu kwenye siasa kwa kuongoza vuguvugu la vijana la YK92, lililopewa jukumu la kuwarai watu kumuunga mkono rais wa wakati huo, hayati Daniel Toroitich Arap Moi. Wapinzani na wakosoaji wake husema huko ndiko alikopata fedha na kuzitumia kufanya biashara, na hadi leo madai ya ufisadi na unyakuzi wa ardhi bado humuandama. Madai ambayo amekuwa akiyakanusha.

Soma pia: Kampeni za uchaguzi zimemalizika nchini Kenya lakini taarifa potofu zaendelea mitandaoni.

Mnamo mwaka 1997, alipojaribu kuwania kiti cha uwakilishi bunge wa eneo lake Eldoret kaskazini, Moi alimwambia kuwa alikuwa mtoto mkosa adabu na mwana wa maskini. Lakini bila ya kuvunjika moyo wala kukata tamaa, Ruto aliendelea na akatwaa kiti hicho ambacho alihifadhi katika chaguzi zilizofuata.

Muuza kuku aingia Ikulu

Ruto akizungumza na waandishi habari mara baada ya kupiga kura yake Agosti 9.Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Licha ya kuandamwa na tuhuma za ufisadi miaka ya kisogoni, Ruto aliyetoka katika familia ya kawaida tu huku yeye mwenyewe akiuza kuku kandokando ya barabara, lakini kwa imani yake alikwea majukwaa ya kisiasa hadi kufikia madaraka ya juu ambapo miaka kumi iliyopita alikuwa naibu rais.

Alitaja kinyang'anyiro kati yake na Raila Odinga kwenye uchaguzi wa Agosti 9 kama ushindani kati ya watu wa tabaka mbili; kina yahe walala hoi aliowaita ‘hustlers' dhidi ya watu wa ‘nasaba' za juu ambazo familia zao zimetawala siasa za Kenya kwa miongo mingi.

Ruto alijitosa kwenye siasa, miongo mitatu iliyopita, na alikuwa naibu rais katika kipindi cha miaka 10 ambapo Rais Uhuru Kenyatta aliiongoza Kenya hadi mwisho wa muhula wake Agosti 2022. Hii ni licha kwamba kulikuwa na msuguano kati ya Uhuru na Ruto katika muhula wa pili na wa mwisho mamlakani.

Soma pia: Muungano mpya wa siasa wazinduliwa nchini Kenya

Tofauti na Uhuru

Ruto, mfanyabiashara huyo aliyetoka katika Maisha ya ukata hadi utajiri, amewania urais kwa mara ya kwanza 2022 wadhifa aliyodhani ilikuwa kibindoni kama zawadi ya kumuunga mkono Kenyatta kwenye chaguzi za mwaka 2013 na 2017.

Ndoa hiyo ya kisiasa iliegemea zaidi masilahi yao kufuatia machafuko mabaya ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008 hasa kati ya jamii ya Wakikuyu-kabila la Kenyatta dhidi ya Wakalenji- kabila la Ruto.

Vigogo hao wawili wa kisiasa walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa tuhuma za kuchochea machafuko ya kikabila Kenya. Hata hivyo kesi hizo zilifutwa huku upande wa mashtaka ukilalamikia kampeni isiyokoma ya vitisho kwa mashahidi.

Ushirikiano na usuhuba wao kisiasa uliokuwa maarufu kama ‘Uhuruto' ulianza kuyumba mwaka 2018, kufuatia ahadi ya Kenyatta kwamba atafanya kazi na Odinga, mpinzani wake wa muda mrefu.

Picha hii inamuonyesha Ruto na aliekuwa mpinzani wake katika uchaguzi, Raila Odinga.Picha: AFP

''Mtu mwenye uzoefu wa kampeni''

Msuguano wao uliendelea kujitokeza hadharani na hata Rais Kenyatta akamtaka ajiuzulu. Kwa upande wake Ruto aliendelea kutoafautiana na bosi wake na hata kupinga azma ya Kenyatta na Odinga kutaka katiba ifanyiwe marekebisho. Azma hiyo ilifeli, ikatizamwa kuwa ushindi kwa Ruto.

Soma pia: Odinga awa rasmi mpizani wa Ruto

"Machoni pa wengi, Ruto hutizamwa kama mmoja wa wapanga mikakati Madhubuti katika siasa za Kenya. "Ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kuendesha kampeni, , mwenye uwezo wa kuona siasa za pande zote mbili. Alisimama na Odinga, alisimama na Kenyatta, anajua nguvu na udhaifu wao" amesema Nic Cheeseman, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Birmingham.

''Sasa nina kitu ''

Wachambuzi wa siasa wanatizama hali ya Ruto kuwa na msukumo wa juu wa mambo kutokana na ukweli kwamba amelazimika kuhangaika kupata kila kitu ambacho amefanikiwa kuwa nacho maishani tokea mwanzo wake katika familia maskini kule Bonde la Ufa Kenya, asili ya jamii ya Kalenjin.

""Niliuza kuku kwenye kivuko cha reli karibu na nyumbani kwangu nikiwa mtoto... niliwalipia ndugu zangu karo ya shule ,Mungu amekuwa mwema kwangu na kupitia bidii na dhamira, sasa nina kitu," Ruto aliwahi kusema hivyo.

Utajiri wake sasa unasemekana kufikia mamilioni ya dola, akiwekeza kwenye hoteli, nyumba sekta ya bima, pamoja na ufugaji wa kuku.