1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto kuwania kiti cha Urais kupitia chama cha UDA

Shisia Wasilwa21 Juni 2021

Makamu wa Rais nchini Kenya William Ruto kwa mara ya kwanza amefichua kuwa atakitumia chama cha United Democratic Alliance kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kenia Präsident William Ruto
Picha: picture-alliance/Photoshot/P. Siwei

Makamu wa Rais nchini Kenya William Ruto kwa mara ya kwanza amefichua kuwa atakitumia chama cha United Democratic Alliance kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ruto ambaye amekuwa akiwatumia washirika wake kunadi chama hicho sasa anasema kuwa, chama cha Jubilee kimepasuka. 

Tamko la Ruto linajiri wakati chama tawala cha Jubilee kikiingia mkataba na chama cha ODM kwa lengo la kumpa nafasi mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao. Uamuzi wa chama cha Jubilee umechukuliwa baada ya mahakama kuamua kuwa Mpango wa Maridhiano ya taifa-BBI ni kinyume cha sheria. Ruto amejitokeza kuwa mpinzani mkuu wa BBI.

Soma zaidi: Hofu ya kuzuka ghasia Kenya yaibuka

Hayo ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa hatamuungua mkono makamu wake kuwania kiti hicho cha urais, na badala yake kusema kuwa ataunga mkono mmoja wa wagombeaji wa Muungano Mkuu wa Upinzani-Nasa iwapo watakuwa na ushirikiano, hatua ambayo inamtenga Ruto kwenye kinyanganyiro hicho kinachozidi kushika kasi. Muungano wa NASA, uliowajumuisha vigogo wa siasa, ulivunjika baada ya chama cha Jubilee kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Ruto anasema hatatetereka kwenye azma hiyo yake.

"Sisi tunataka kuwaambia warafiki zetu kuwa tuko masaa, na tuko rada na tuko chonjo kwa sababu wamekwama na hiyo chama yote. Sisi tutakuwa na chama cha kitaifa ambacho Wakenya wote watatoshea."

Akiwahutubia wakazi wa jimbo la Pokot Magharibi katika eneo la Kapenguria, Ruto hakusita kukilimibikizia chama cha Jubilee lawama kwa kukosa maono, huku akiahidi kuunganisha taifa kabla ya uchaguzi mkuu ujao na kuvisuta vyama vingine ambavyo alidai vinaendekeza ukabila.

Kuna hali ya wasiwasi katika kambi ya Ruto, baada ya tamko la Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu mrithi wake, na sasa kambi hiyo inahofia huenda vyombo vya dola vikatumika dhidi yake kwenye uchaguzi huo mkuu, hivyo kumlemaza. Mpasuko unaoonekana katika eneo la mlima Kenya, ngome ya rais Kenyatta huenda ukawa ni nafuu kwa Ruto ambaye anaonekana kuungwa mkono na baadhi ya viongozi na wakazi.

Hata hivyo ikiwa imesalia miezi 13 kwa uchaguzi mkuu kuandaliwa, huenda hesabu zake zikapanguliwa kwani, historia inaonesha kuwa eneo hilo la Milima Kenya halijawahi kumpigia kura mgombea wa urais kutoka jimbo lingine. Washirika wa Ruto wanazidi kumpigia debe huku baadhi ya wafuasi wa Rais Kenyatta katika ngome yake wakiona kuwa amemsaliti makamu wake aliyesimama naye tangu mwazo.

Iwapo mkataba wa ushirikiano kati ya vyama hivyo utaheshimiwa vyama vya Jubilee na ODM vitakuwa na mgombea mmoja wa rais. Ruto amenukuliwa akisema yuko tayari kumenyana naye. Hata hivyo Raila hajatangaza iwapo atawania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Licha ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza marafuku ya mikutano ya hadhara ya kisiasa kufanyika kwa sababu ya maambukizi ya virusi vya corona, wanasiasa wanaonekana wakipuuza marufuku hiyo, huku macho yao yakilenga uchaguzi mkuu ujao.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW