1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto mwenyekiti mpya wa EAC

Veronica Natalis
30 Novemba 2024

Mkutano wa 24 wa kilele wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika huko Arusha Jumamosi ulimuidhinisha Rais wa Kenya William Ruto, kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.

Rais wa Kenya William Ruto akiwasili Arusha kwa mkutano wa kilele
Rais wa Kenya William Ruto akiwasili Arusha kwa mkutano wa kilelePicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Ruto anachukua kijiti kutoka kwa mwenyekiti anayeachia muda wake Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr.

Katika hotuba yake ya kukabidhi nafasi hiyo Rais Salva Kirr alisema kwamba ilikuwa ni wakati mzuri kwake kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Huduma ya mwaka mmoja kama mwenyekiti

Kiir vile vile alisema ana imani kuwa majadilianoya kuijenga Jumiya imara yataendelea chini ya mwenyekiti mpya.

Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

"Ninaamini kwamba mikakati thabiti ya kuendeleza amani na usalama miongoni mwa nchi zetu itaendelea, ni Sudan Kusin itaendelea kutoa ushirikiano,” alisema Kirr.

 Rais William Ruto atashikilia nafasi hiyo ya mzunguko  kwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Majukumu yarais huyo wa Kenya kama ilivyo katika mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni kuratibu shughuli za Jumuiya, kusimamia utekelezaji wa maamuzi, kuhamasisha mshikamano na kusimamia mchakato wa ujumuishaji.

Ruto alimpongeza mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais wa Sudan Kusin Salva Kirr kwa uongozi mzuri.

"Hongera sana Mheshimiwa, umetuheshimisha wote hapa,” alisema Ruto.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki pia umeiidhinisha lugha ya Kifaransa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya hiyo kongwe barani Afrika, ikiifuatia lugha ya Kiswahili iliyoidhinishwa hivi karibuni, kutumika katika mataifa nane wanachama yenye idadi ya watu wanaofikia milioni 300 mpaka sasa.

Kabla ya hapo,  lugha ya Kingereza pekee ndio ilitambulika kuwa lugha rasmi ya Jumuiya  hiyo.

Mjadala wa ubunifu wa mabadiliko ya kidijitali

Mkutano wa 24 wa kawaida wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliwaleta pamoja viongozi wa mataifa nane yanayounda Jumuiya hiyo mpaka sasa.

Viongozi wa EAC wakiwa kwenye mkutano wa kilele huko ArushaPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Mkutano huo ulifanyika chini ya kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo ni jukwaa la kutathimini mafanikio ya miongo miwili na nusu iliyopita, huku ukipanga mikakati ya kuimarisha mshikamano zaidi wa kikanda.

Viongozi hao waliokutana Arusha kaskazini mwa Tanzania yalipo makao makuu ya Jumuiya hiyo, pia wamejadili jukumu la ubunifu wa mabadiliko ya kidijitali katika kuchochea maendeleo endelevu na kutekeleza dira ya Jumuiya hiyo kuelekea mwaka 2050.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW