Rwanda: Christopher Kayumba akanusha madai dhidi yake
24 Machi 2021Siku moja tu baada ya kutangaza kuunda chama cha upinzani cha Rwandese Platform for Democracy (RPD) ambacho hakijasajiliwa, Dr Christopher Kayumba alidaiwa kujaribu kumbaka mwanafunzi wake alipokuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Tuhuma hizo zilienezwa na aliyejiita Kamaraba Salva kupitia mtandao wa Twitter, akisema anaozungumza kwa niaba ya rafiki yake aliyedai aliponea chupuchupu jaribio la kumbaka.
Idara ya Taifa ya Upelelezi (RIB) ilianza kumfuatilia Dkt Kayumba, na jana alijitokeza kutoa majibu kuhusu kesi hiyo ambayo amesema anaamini ina misukumo ya kisiasa.
"Hiyo ni propaganda iliyolenga kuniaibisha, wanasema nilijaribu kumbaka msichana huyo mwaka 2017 inawezekanaje nahojiwa leo? Mwaka 2019 walinibambikizia kesi ya kusababisha vurugu katika uwanja wa ndege, kama nilifanya kosa hilo miaka miwili kabla kwa nini hawakuniuliza kuhusu ubakaji huo kipindi hicho? Jiulize kwa nini wamezua mambo hayo tulipoanzisha chama chetu, na siyo mimi tu hata katibu wetu Nkusi Jean Bosco wamemkamata eti ni mwizi.”alisema Dkt Kayumba
Idara ya taifa ya Upelelezi yatupilia mbali madai ya Kayumba
Hata hivyo, Msemaji wa Idara ya Taifa ya Upelelezi (RIB) Dkt Thierry Murangira, ametupilia mbali madai hayo akisema RIB hufanya kazi kwa ustadi bila kuegemea upande wowote.
"Haihusiani na chama chake na wala haihusiani na mwanaume huyo ambaye inasemekana ni mwanachama wa chama chake, tulipomkamata hatukujua ana fungamano lolote na Kayumba. Yeye na watu wengine watano walimtishia maisha mfanyabiashara mmoja huko Gakinjiro wakijiita maafisa wa Polisi na Mamlaka ya Mapato, na kumtaka awape faranga miliyoni kumi. Sisi tunachapa kazi kwa uhuru bila kupewa miongozo na watu wa nje, na tunamfuatilia yeyote ambaye ametenda maovu bila kujali yuko chama gani au anafanya kazi gani,” alisema Dkt Thierry Murangira
Disemba mwaka jana, Bwana Kayumba alirudi uraiani baada ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela alichohukumiwa baada ya kukutwa na hatia ya kusababisha fujo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigali.
Mwezi huu alikiasisi chama cha Rwandese Platform for Democracy ambacho amesema miongoni mwa malengo yake ni kuimarisha demokrasia huku akiwalaumu viongozi wote walioiongoza Rwanda tangu kupata uhuru mwaka 1962 kwa kushindwa kuwavumilia wapinzani, akisema hiyo ndiyo sababu ya uwepo wa makundi ya waasi kama FDLR na FLN yanayolenga kuiangusha serikali.
Kauli hiyo kwa namna moja ama nyingine inatilia mkazo hoja za wanasiasa wenzake wa upinzani akiwemo Victoire Ingabire na Bernard Ntaganda ambao wamekuwa wakilaumu serikali kwa kushindwa kuweka mazingira ya uhuru wa maoni na kukataa kusajili vyama vyao ambavyo vimekuwepo kwa muda wa zaidi ya miaka 10.
Mwandishi: Janvier Popote/DW, Kigali.