Rwanda hatiani kuhusu uhuru wa kujieleza
23 Desemba 2021Akielezea sheria zinazokinzana, Mkurugenzi Mtendaji wa The Legal Aid Forum, Andrews Kananga amesema ni sheria inayosimamia vyombo vya habari inayosema vifaa vya mwandishi wa habari haviwezi kukamatwa, huku sheria inayosimamia Idara ya Taifa ya Upelelezi ikimpa mpelelezi haki ya kukamata kila kitu kinachoweza kufanikisha kazi yake bila kujali ni cha nani.
Mwaka 2013 Rwanda iliweka sheria ya kupata habari ikiwa ni nchi ya 11 duniani kwa kuwa na sheria kama hiyo. Hata hivyo, utekelezaji wake ni finyu, kwa mujibu wa Bwana Jean Baptiste Hategekimana, Mtafiti na Mhadhiri wa Uandishi wa Habari, ambaye ni miongoni mwa watunzi wa ripoti hii.
"Ni sheria isiyokuwa na adhabu kwa ambaye amekataa kutoa habari, inasema aripotiwe kwa Ofisi ya Ombudsman lakini Ombudsman hatakupiga hata faini. Kingine tulichokiona, maafisa wa serikali za mitaa huminya uhuru wa maoni kwa raia wasiokuwa wasomi kwa kujiaminisha kwamba hawajui haki zao huku wakiogopa kuwakandamiza wasomi maana anajua kama mimi akitenda kosa najua kujitetea'',alisema Hategekimana.
''Kama habari hiyo nimeijua leo itakuwaje ?''
Scovia Mutesi ni mwandishi wa habari mjini Kigali, katika mazungumzo na DW ameeleza anavyotaabika kupata habari si kwa watendaji wa serikali za mitaa tu, bali hata katika ngazi za juu za uongozi wa nchi.
"Huwezi kuomba habari Benki ya Taifa ama Wizara ya Fedha na Mipango ukapata, utamaduni wa kutoa habari hawana kabisa. Lakini pia ukienda mahakamani wanakuambia kama unataka kurekodi sauti ama kupiga picha katika chumba cha kusikilizia kesi unaomba kibali masaa 48 kabla, jiulize kama habari hiyo nimeijua leo itakuwaje?”,alihoji Mutesi.
Mahakama maalumu ya kesi za kesi za wanahabari
Peacemaker Mbungiramihigo ni Mchambuzi wa Sera ya Vyombo vya Habari katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Anasema tafiti mbalimbali zimeonesha mapungufu kama haya na serikali imeanza kuyashughulikia.
"Tumeanza kuirekebisha sera ya vyombo vya habari ya mwaka 2011 ambayo imepitwa na wakati, lazima viongozi watoe habari na asiyetii sheria kuwe na adhabu.”,alisema Mburingamihigo.
Waliotunga ripoti hii wamependekeza kuwekwa mahakama maalum ya kuendesha kesi zinazohusiana na utoaji habari wakisema mahakama zilizopo zina mahakimu wasioelewa taaluma hiyo.