Rwanda, Kongo zakubaliana kukomesha uhasama
19 Machi 2026
Mazungumzo ya siku mbili yaliyofanyika mjini Washington kati ya wawakilishi wa Rwanda na Kongo yalimalizika Jumatano (Machi 18) kwa pande hizo kutoa tamko la pamoja ambalo kila upande umeahidi utayarifu wake wa kuendelea na mchakato wa amani na kupunguza misuguano baina yao.
Kwa mujibu wa tamko hilo lililosambazwa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani hapo jana, Kongo na Rwanda "zimekubaliana kuchukuwa hatua kadhaa za pamoja zikiwemo zile zinazohakikisha heshima na mamlaka ya kila upande yanadumishwa."
"Rwanda kutokujihusisha ama kuacha harakati za kijeshi kwenye maeneo yanayotambulika kuwa ni ya Kongo, na Kongo kuongeza juhudi zenye kuhakikisha kundi la waasi la FDLR linadhibitiwa, na pia pande zote kuwalinda raia wote." Lilisema tamko hili wakati likitaja baadhi ya hatua hizo.
Kundi la FDLR, ambalo Rwanda inaituhumu Kongo kuliunga mkono, liliundwa na wanamgambo wa Kihutu waliokimbilia Kongo baada ya kuhusika na mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, mauaji ambayo yaliangamiza takribani watu milioni moja wa jamii ya Kitutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Kundi la waasi la M23, ambalo Kongo inaituhumu Rwanda kuliunga mkono, linasema linaendesha vita mashariki mwa Kongo kwa lengo la kuzilinda jamii zenye asili ya Kitutsi kwenye eneo hilo.
Marekani yaishinikiza Rwanda
Mkutano huu ulioanza Jumanne na kumalizika Jumatano ulikuwa wa kwanza kati ya pande hizo tangu Wizara ya Fedha ya Marekani ilipotangaza vikwazo dhidi ya Jeshi la Rwanda na maafisa wanne wa ngazi za juu mnamo Machi 2.
Washington inaishutumu Kigali kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23, kundi lenye nguvu kubwa mashariki mwa Kongo na ambalo limefanikiwa kuyateka na kuyakalia maeneo makubwa na muhimu kwenye eneo hilo tangu Januari 2025. Rwanda inazikanusha tuhuma hizo.
Rwanda na Kongo zilisaini makubaliano ya amani mjini Washington mwezi Disemba kama sehemu ya shinikizo la Rais Donald Trump kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka wawekezaji wa mataifa ya Magharibi.
Lakini siku chache baadaye, waasi wa M23 waliingia kwenye mji wa Uvira ulio mpakani mwa Kongo na Burundi, ingawa waliondoka baadaye kutokana na shinikizo la Marekani.
Lakini mapema mwezi huu, Washington ilisema kuendelea kuwapo kwa waasi hao kwenye eneo hilo la mpakani kunahatarisha kuutanuwa zaidi mzozo wa mashariki mwa Kongo kuwa wa kikanda.