1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda kujenga kinu cha nyuklia kuzalisha umeme

13 Septemba 2023

Serikali ya Rwanda imetia saini hapo jana makubaliano na shirika kutoka mataifa ya Canada na Ujerumani, ili kuanzisha ujenzi wa kinu cha nyuklia ambacho kitakuwa tayari kwa majaribio ifikapo mwaka 2026.

Russland | Baustelle Atomkraftwerk Kursk II
Ujenzi wa Kinu cha Nyuklia mjini Kurchatov, Urusi:02.11.2022Picha: Tatyana Simonenkova/TASS/IMAGO

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya "Dual Fluid Energy", Goetz Ruprecht amewaambia waandishi wa habari mjini Kigali kuwa  " aina mpya ya vinu hivyo, vinaweza kutumiwa kuzalisha umeme, haidrojeni na mafuta yaliyosindikwa kwa gharama ndogo kuliko mafuta ya visukuku.

Waziri wa miundombinu wa Rwanda Ernest Nsabimana amesema matumizi ya nishati ya nyuklia yatatoa chanzo thabiti na cha kuaminika cha umeme, kupunguza utegemezi wa mafuta na kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati.

Nsabimana amendelea kuwa kujumuisha nyuklia katika jumla ya vyanzo vya nishati kutapelekea kuwa na aina mbalimbali za vyanzo vya nishati, kuimarisha usalama wa nishati na kupunguza hatari ya uhaba wa usambazaji.

Soma pia: Matumizi ya nishati mbadala nchini Rwanda

Awali mnamo mwaka 2019, Rwanda ilitia saini mkataba wa kuanzisha vinu vya nyuklia kwa ushirikiano na wakala wa nyuklia wa Urusi "Rosatom", jambo lililozusha upinzani mkali hasa kuhusu hatari zinazohusiana na masuala ya kiusalama.

Upinzani nchini Rwanda: Mradi huo unayaweka maisha ya raia wa Rwanda hatarini.

Cyprien Bigirimana, fundi wa matengenezo, akiwa katika mitambo ya kuchimba gesi ya methane kwenye Ziwa Kivu, kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha "Kivuwatt" huko Kibuye, Wilaya ya Karongi, katika Mkoa wa Magharibi wa Rwanda, Novemba 1, 2021. Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Rais wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha "Democratic Green Party of Rwanda", Frank Habineza, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya "Dual Fluid Energy" ni hatari na kwamba hayana tofauti kubwa na makubaliano ya mwaka 2019 kati ya serikali ya Kigali na wakala wa nyuklia kutoka Urusi.

Habineza amesisitiza : " Hakuna utafiti unaoweza kunishawishi kuwa kuna mahali katika nchi hii (Rwanda) ambapo kinu cha nyuklia kinaweza kujengwa bila kuyaweka maisha ya watu hatarini."

Bodi ya Nishati ya Atomiki ya Rwanda  ikishirikiana na Kampuni hiyo wamebaini kuwa miradi yao ni salama na wala si tishio kwa watu au mazingira. Katika taarifa yao ya pamoja wameeleza: " Kinu chetu cha majaribio ni kifaa kidogo chenye chembechembe ndogo za mionzi. Kwa sababu hii, maradi huu si tishio kwa mazingira."

Taarifa hiyo imeendelea kwa kusema: " Kwa mfano, hata ikitokea mripuko kwenye kinu hicho au kwenye jengo lenyewe, basi ni kiwango kidogo mno cha mionzi ndicho kitakachotawanyika."

Afrika Kusini ndio nchi pekee barani Afrika iliyo na mpango wa nyuklia wa kiraia, na vinu vyake viwili vimekuwa vikifanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 na kuzalisha megawati 1,860 za umeme, ikiwa ni sawa na karibu 4% ya nishati yote inayozalishwa nchini humo.

(AFPE)