Rwanda: Serikali ya Kongo ilaumiwe kukamatwa mji wa Uvira
11 Desemba 2025
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe amesema kitendo cha jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoliunga mkono maarufu kama Wazalendo kuendelea kuzishambulia ngome za waasi na waasi hao kujibu mashambulizi kwa kuyakamata maeneo zaidi, kinaufanya mzozo huo kuwa na utata zaidi.
Kauli ya Nduhungirehe ameitoa wakati ambapo Marekani na nchi za Ulaya zikiendelea kuweka shinikizo kubwa dhidi ya Rwanda kwa kile wanachokisema kuwa Rwanda inakiuka mkataba wa Washington ambao ulizitaka pande hizo mbili kusimamisha mapigano. Jana waasi wa M23 waliukamata mji wa kimkakati wa Uvira karibu na mpaka wa Kongo na Burundi ambao ni watatu uliokamatwa na waasi hao mwaka huu baada ya Goma mji mkuu wa Kivu Kaskazini na Bukavu makao makuu ya jimbo la Kivu Kusini.
Mkataba wa Washington ulitabiriwa kurejesha amani
Katikati mwa mzozo huo, mkataba wa Washington uliosainiwa December 4 ulipewa matumaini makubwa ya kusitisha mapigano hayo. Hata, mkataba huo haujadumu hata wiki moja kabla ya mji wa Uvira kukamatwa na waasi na kusababisha taharuki hata kwa jamii ya kimataifa. Sasa waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier amesema kupitia kwenye televisheni ya taifa kwamba mzozo huu unachangiwa na serikali ya Kongo kutokana na kushindwa kuwajibika
"Tuliweka saini katika rasimu ya mkataba wa amani tarehe 27 June mjini Washington, lakini pia kuna mkataba wa amani wa Doha, haya makubaliano na mikataba yote inazitaka pande zote kusimamisha mapigano, lakini tangu wakati huo hadi hii leo kila siku sisi kama Rwanda tumekuwa tukipiga kelele kuhusu mashambulizi ya jeshi la Kongo kwa kutumia silaha nzito na droni kwenye maeneo ya waasi, hakuna siku hata moja ambayo hatujaacha kuarifu jamii ya kimataifa kuhusu hatari inayosababishwa na mienendo ya serikali ya Kinshasa.Lakini pia kwanashambulia makazi ya raia wa kinyamurenge pamoja na matumizi ya lugha za chuki."
Taharuki yatanda eneo la Maziwa Makuu na Burundi
Taharuki imetanda katika eneo la Maziwa Makuu na Burundi kwa upande wake imesema inatathmini athari za matatizo hayo huku ikilaumu Rwanda kusababisha matatizo na kufunga mpaka wake na Kongo. Nchi za Ulaya na Marekani zinaendelea kutoa kauli kali kuitaka Rwanda kusitisha msaada wake kwa kundi la M23 na kuyaondoka majeshi yake mashariki mwa Kongo suala ambalo hadi sasa Rwanda inaendelea kulikanusha kuwa haina majeshi kule.
Kwa upande mwingine wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa ikiwa hakutachukulia juhudi za makusudi kusimamisha mapigano huenda nchi za kanda ya maziwa zikajikuta katika mzozo wa kivita awali Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alitishia kuishambulia Rwanda ikiwa waasi wa M23 wangeuteka mji wa Uvira akisema kutekwa kwa Uvira ni sawa na kuuteka mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.