Rwanda kuwahamishia kwingine wakimbizi wa Burundi
12 Februari 2016Taarifa kutoka Rwanda imesema serikali itaanza mara moja kushirikiana na washirika wake katika jumuiya ya kimataifa kupanga jinsi ya kupelekwa kwa wakimbizi wa Burundi katika nchi nyingine. Haijabainika wazi Rwanda ina mipango ya kuwahamishia wakimbizi kwenye mataifa gani.
Rwanda imeongeza kusema kuwa iko tayari kushughulikia wajibu wake wa kuwalinda na kuwajali wakimbizi lakini historia ya mizozo katika kanda ya Maziwa Makuu na kuwepo wakimbizi kutoka nchi jirani kunasababisha kuwepo kwa athari kubwa kwa nchi zinazohusika katika kuwashughulikia wakimbizi.
Wiki iliyopita, wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliliarifu Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa Rwanda imewasajili na kuwapa mafunzo wakimbizi kutoka Burundi miongoni mwao watoto kwa lengo la kutaka kumng'oa madarakani Rais Pierre Nkurunziza.
Rwanda yahusishwa na mzozo wa Burundi
Siku ya Jumatano, Marekani iliishutumu Rwanda kwa kuhusika katika visa vya kuliyumbisha taifa la Burundi. Mjumbe wa Marekani katika kanda ya Maziwa Makuu, Thomas Perriello, amesema kuna taarifa za kuaminika za kusajiliwa kwa wakimbizi wa Burundi walioko katika kambi za Rwanda ili wahusike katika mashambulizi yanayofanywa na makundi yanayoupinga utawala wa Burundi.
Mara kwa mara, Burundi imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wanaotaka kuipindua serikali ya Rais Nkurunziza, madai ambayo Rwanda imeyakanusha vikali.
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Louise Mushikwabo, amesema hali ya kutojali vyanzo vinavyojulikana wazi vinavyosababisha msukosuko Burundi na mmiminiko wa wakimbizi ni jambo linalotia wasiwasi.
Mushikwabo amesema kitisho kinachozidi dhidi ya utawala wa kitaifa Rwanda kutokana na mzozo wa Burundi na tofauti kati ya nchi hizo mbili kuhusu uhusiano wa mambo ya kigeni, ni jambo lisilokubalika.
Mbali na Rwanda, nchi nyingine jirani pia zinawahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi. Tanzania inawahifadhi wakimbizi 130,000, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ina zaidi ya wakimbizi 18,000 na Uganda ambayo inapakana na Burundi upande wa kaskazini ina wakimbizi 21,000.
Ghasia zaendelea Burundi
Huku hayo yakijiri, ghasia zimeendelea nchini Burundi. Hapo jana mripuko wa guruneti uliwajeruhi watu 26 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura, huku tisa kati yao wakijeruhiwa vibaya.
Wakati huo huo, Ufaransa inashauriana na nchi nyingine wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu azimio jipya ambalo litapelekea kujihusisha zaidi kwa jumuiya ya kimataifa katika mzozo huo wa Burundi.
Uingereza imesema huenda azimio hilo likahusisha kupelekwa kwa polisi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Burundi imekuwa katika mzozo tangu Rais Nkurunziza kutangaza azma ya kugombea muhula mwingine madarakani mnamo mwezi Aprili mwaka jana.
Mamia ya watu wameuawa tangu mzozo huo kuzuka na takriban wengine 230,000 wametorokea nchi jirani. Kulingana na shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, kiasi ya wakimbizi 75,000 kati yao wako nchini Rwanda.
Mwandishi: Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Mohammed Khelef