1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda, Mauritania zathibitisha kesi za kwanza za Corona

Sekione Kitojo
14 Machi 2020

 Mataifa ya  Afrika ya rwanda  na  Mauritania  yametangaza kesi za  kwanza  za  maambukizi  ya  virusi  vya  Corona. Wizara  ya afya  ya  rwanda  imesema  raia  wa  India amethibitishwa  kuwa  na virusi  vya  Corona.

Afrika Senegal Coronavirus Pasteur Institute in Dakar
Picha: Getty Images/AFP/Seyllou

Wizara  ya  afya  ya  taifa  hilo  la  Afrika  ya  kati  limesema  katika taarifa  leo(14.03.2020) kwamba  mtu  huyo  alikuwa  anaonesha ishara  za  ugonjwa  huo  wakati  alipowasili  nchini  Rwanda akitokea  katika  mji  wa  Mumbai  nchini  India  hapo Machi 8. Taarifa   ya  wizara  hiyo  imesema  Machi 13  mtu huyo  alifika mwenyewe  katika  kituo  cha  afya  ambako  mara  moja  alifanyiwa uchunguzi  na  sasa  yuko  katika  hali  nzuri.

Maabara ya taasisi ya Pasteur mjini Dakar Senegal , wataalamu wakifanya utafiti wa virusi vya CoronaPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Taifa  la  Afrika  magharibi  la  mauritania  limethibitisha  kesi  ya kwanza  ya  virusi  vya  corona mtu huyo  akiwa  mgeni ambaye aliingia  nchini  humo Machi 9 akitokea  barani  Ulaya. Waziri  wa afya  Mohamd Nazir Ould Hamid  amesema  jioni  Ijumaa  kuwa mgonjwa  "aliondolewa  mara  moja  na  hatua  zote  za  kiafya zimechukuliwa  kumtibu na  kudhibiti  kesi  hiyo  ya  kwanza  ya virusi  vya  corona  nchini  humo."

Virusi vya  corona  vinasambaa  katika  nchi  nyingi  za  Afrika. Kenya , Guinea  na  Ethiopia  zimeripoti kesi  zao  za  kwanza  siku ya  Ijumaa, wakati Gabon na  Ghana zimefanya  hivyo  jioni  ya Alhamis. Sudan pia  imeripoti kesi  ya  kwanza  ya  muathirika  wa virusi  vya  corona ambaye  amefariki.

Nchi 19  kati  ya  54  barani  Afrika  zimeripoti  kesi  za  virusi  vya corona. Maafisa  wanasema  nyingi  ya  kesi  hizo ni  kutoka  mataifa ya  kigeni.

Baada ya  kujifungia  ndani  chini  ya  sheria  nchini  Italia  ya kutoruhusu  watu  kutembea  ovyo  nchi  nzima ili  kupambana  na virusi  vya  corona, mamilioni  ya  Wataliani wameamka  leo Jumamosi  wakijikuta wamenyimwa  moja  ya  burudani  ya  kawaida iliyobaki, kutemea  katika  maeneo  nje ya  nyumba  zao.

Watu wanashauriwa kuosha mikono kila maraPicha: Imago Images/M. Westermann

Sehemu za wazi za michezo zafungwa

Meya  ya  miji , ikiwa  ni  pamoja  na  Roma  na  Milan, waliamua ilipofika  jioni  ya  Ijumaa kufunga  sehemu  za  kucheza watoto pamoja  na maeneo ya  wazi. Maafisa  wa  afya  wamelalamika kuwa  watu  wengi  mno wanajikusanya  pamoja, iwapo ni  kucheza mpira, ama  kufanya  mazowezi  ya kukimbia  katika  makundi.

Chini  ya  amri  ya  serikali  iliyotolewa  mapema  wiki  hii, watu waliruhusiwa  kufanya  matembezi, kufanya  mazowezi  wa  kukimbia ama  kuendesha  baisikeli  katika  maeneo  ya  wazi  iwapo tu watakaa  mbali  mbali  kati  ya  mtu  na  mtu. Lakini  hakuna  mtu aliyetekeleza  sheria hiyo.

New Zealand, Cambodia  na  Taiwan  ni  miongoni mwa  nchi  katika eneo  la  Asia  Pacific  kutangaza  vizuwizi  vipya  vya  usafiri siku ya  Jumamosi  kama  sehemu  ya juhudi za  dunia kuzuwia kusambaa  kwa  virusi  vipya  vya  corona.

Kila  mtu  anayeingia New Zealand kuanzia kesho  Jumapili itabidi atengwe kwa  muda  wa  siku 14, waziri  mkuu Jacinda Ardern amesema  katika  mkutano  na  waandishi  habari. Ameongeza  kuwa ni  wasafiri  tu  kutoka  katika  kisiwa  hicho  cha  bahari  ya  Pacific ambao  hawatahusika  na  sheria  hiyo.

Maafisa wa afya wakimpokea mgonjwa aliyeambukizwa virusi vya Corona mjini Wuhan ChinaPicha: picture-alliance/Photoshot/Xiao Yijiu

Amewataka  raia  wa  New Zealand  kuepuka  safari  ambazo  si lazima  nje  ya  nchi na  kusema  meli  za  safari  za  watalii hazitaruhusiwa  kutia  nanga  katika  bandari  za  nchi  hiyo  hadi Juni 30.

Uhispania  inajitayarisha  kutangaza hali  ya  hatari leo Jumamosi (14.03.2020) na  Italia  inaimarisha  hatua  yake  ya  kuwazuwia watu  kutoka  majumbani  mwao kwa  kufunga  maeneo  ya  burudani ya  wazi, wakati  Denmark  na  Poland  zimekuwa  nchi  za  hivi karibuni  kufunga mipaka yao kwa  wasafiri  katika  juhudi  za kupunguza  kasi  ya  kusambaa  kwa  virusi  vipya  vya  Corona.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW