Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimekubaliana kumaliza uhasama unaosababishwa na makundi ya uasi. Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye mkutano wa kilele uliofanyika Luanda, Angola jana Jumatano.
Matangazo
Taarifa ya ofisi hiyo ya rais wa Congo imesema kwenye mazungumzo hayo ya pande tatu, wakuu wa mataifa hayo Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Paul Kagame wa Rwanda na mwenyeji wa mazungumzo rais Joao Lorenco wa Angola wamekubaliana kusitisha uhasama mara moja na kulitaka kundi la wanamgambo wa M23 kujiondoa nchini Congo. Aidha mazungumzo yaliyozorota kuhusu mahusiano kati ya Rwanda na Congo yataanzishwa upya mjini Luanda Julai 12.
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ni kuhakikisha kwamba wanalikabili kundi la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda, FDLR. Kundi hilo la wanamgambo wa kabila ya Hutu linashutumiwa na Kigali kuendesha mapambano kwa kushirikiana na jeshi la Congo, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa ofisi ya rais wa Rwanda jana jioni.
Baada ya mkutano huo rais wa Rwanda Paul Kagame alisema anatarajia makubaliano hayo yatatekelezwa na mataifa hayo kurejea katika hali ya kawaida.
Amesema "Pia namshukuru rais Tshisekedi kwa michango yake inayotuwezesha nasi kuchangia ili mambo yasonge mbele na tunatarajia kurejesha mahusiano ya nchi zetu katika hali ya kawaida kwa kutatua pia masuala yanayoendelea huko kwetu ambayo yametufikisha hapa.
Rais Felix Tshisekedi amenukuliwa akisema anaamini mchakato huo utahitimisha haraka uhasama na mapigano na kurejesha utulivu kwenye mataifa hayo.
"Natumaini mchakato huu utasababisha mapigano kusitishwa mara moja na kundi la M23 kuondoka na ninatarajia utekelezaji wa mpango huo unaweza kutufikisha kwenye mchakato wa amani, utulivu na kuaminiana." alisema Tshisekedi.
Hali ya wasiwasi na mivutano ya kidiplomasi iliongezeka kwa kasi kati ya majirani hao wawili tangu kundi la wanamgambo wa M23 kuanzisha mashambulizi makubwa mashariki mwa Congo mwishoni mwa mwezi Machi. Congo imekuwa imishutumu Rwanda kwa kulisaidia kundi hilo. Hata hivyo Kigali inakana shutuma hizo na badala yake iliishambulia Congo kwa kulisaidia kundi la waasi ambalo wanamgambo wake wanadaiwa kushiriki mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, ingawa pia Congo inakana.
Tizama Picha:
Siku 100 za mauaji ya kimbari nchini Rwanda
Rwanda inafanya kumbukumbu ya miaka 25 tangu kutokea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Mauaji hayo bado yanaendelea kuushtua ulimwengu hadi hii leo. Jamii ya kimataifa ilisubiri muda mrefu kusikia kilio cha wahanga.
Picha: Timothy Kisambira
Ishara kwa wenye msimamo mkali
Aprili 6, 1994 washambuliaji wasiojulikana waliidungua ndege ya rais wa Rwanda, Juvénal Habyarimana wakati ikikaribia kutua mjini Kigali. Habyarimana, mwenzake wa Burundi na watu wengine wanane waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walifariki. Siku iliyofuata yalianza mauaji ya kupanga ambayo yalidumu kwa miezi mitatu na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 800,000.
Picha: AP
Mauaji ya kulenga
Baada ya kuuawa kwa rais, Wahutu wenye msimamo mkali walianza kuwachinja Watutsi wachache na Wahutu waliojaribu kuwazuwia. Wauaji walikuwa wamejiandaa vizuri na waliwalenga hasa wanaharakati wa haki za binaadamu, waandishi habari na wanasiasa. Miongoni mwa wahanga wa kwanza tarehe 7 Aprili alikuwa Waziri mkuu Agathe Uwiringiymana.
Picha: picture-alliance/dpa
Uokozi wa wageni
Wakati maelfu ya Wanyarwanda wakiuawa mjini Kigali na vijijini kila siku katika siku zilizofuatia, vikosi maalumu vya Ubelgji na Ufaransa viliwaondoa karibu wageni 3500. Tarehe 13 Aprili askari wa mwavuli wa Ubelgji waliwaokoa pia wafanyakazi 7 wa Kijerumani na familia zao kutoka kituo cha utangazaji cha DW mjini Kigali. Ni wafanyakazi 80 tu kati ya 120 wenyeji walionusurika mauaji hayo.
Picha: P.Guyot/AFP/GettyImages
Kilio cha msaada kisichosikilizwa
Mapema Januari 1994, Kamanda wa UNAMIR Romeo Dallaire alitaka kuchukua hatua kufuatia taarifa ya njama ya kuwamaliza Watutsi. Onyo alilolituma katika Umoja wa Mataifa Januari 11, ambalo baadaye lilikuja kujulikana kama "Fax ya mauji ya Kimbari" halikuzingatiwa. Na maombi yake kwa naibu katibu mkuu anaeshughulikia ulinzi wa amani Kofi Annan baada ya kuanza kwa mauaji ya kimbari yalikataliwa.
Picha: A.Joe/AFP/GettyImages
Vyombo vya habari vya chuki
Kituo cha Redio cha Mille Collines (RTLM) na gazeti la kila wiki la Kangura vilichochea chuki dhidi ya Watutsi. Mwaka 1990, Kangura lilichapicha "Amri 10 za Wahutu" za ubaguzi. Redio Mille Collines, maarufu kwa vipindi vya muziki na michezo iliwachochea Wahutu kuwasaka na kuwauwa Watutsi. Muongozaji Milo Rau aliandaa filamu yake ya "Hate Radio" kwa ukumbusho wa vipindi hivyo vya kikatili.(picha)
Picha: IIPM/Daniel Seiffert
Hifadhi katika Hotel
Mjini Kigali Paul Rusesabagina aliwaficha zaidi ya watu 1000 katika hotel ya Mille Collines. Rusesabagina alikuchuwa nafasi ya Meneja wa Kibelgji alieondoka nchini humo. Kwa kutumia vileo na pesa, aliwazuwia wanamgambo wa Kihutu kuwauwa wakimbizi. Katika maeneo mengine mengi ambako watu walitafuta hifadhi, hawakuweza kunusurika na mauaji.
Picha: Gianluigi Guercia/AFP/GettyImages
Mauaji ndani ya makanisa
Kanisani hapakuwa tena mahala patakatifu. Karibu wanaume, wanawake na watoto 4000 waliuawa kwa mashoka, visu na mapanga katika kanisa la Ntarama karibu na mji wa Kigali. Hii leo Kanisa hilo ni moja ya vituo vingi vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari. Mafuvu yaliyopangana, mifupa na matundu ya risasi kwene kuta ni ukumbusho wa mauaji ya kimbari.
Picha: epd
Ushiriki wa Ufaransa
Serikali mjini Paris iliendeleza uhusiano wa karibu na utawala wa Kihutu. Jeshi la Ufaransa lilipoingilia kati mwezi Juni, liliwawezesha wanajeshi na wanamgambo waliohusika na mauaji ya kimbari kukimbilia nchini Zaire - sasa DRC, na liliwaruhusu kuondoka na silaha zao. Hadi sasa wanaendelea kuwa tishio kwa usalama wa Rwanda.
Picha: P.Guyot/AFP/GettyImages
Mtiririko wa wakimbizi
Wakati wa mauaji ya kimbari, mamilioni ya Wahutu na Watutsi walikimbilia nchini Zaire, Tanzania na Uganda. Milioni mbili kati yao walikimbilia Zaire peke yake. Walihusisha maafisa wa zamani wa jeshi na wachochezi wa mauaji, ambao baadaye waliazisha kundi la uasi la ukombozi wa Rwanda FDLR, ambalo linaendelea kuwafanyia ukatili wakaazi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo hadi sasa.
Picha: picture-alliance/dpa
Kutekwa kwa mji wa Kigali
Tarehe 4 Julai waasi wa kundi la Rwandan Patriotic Front RPF, walikuwa wanafanya doria katika eneo la karibu na Kanisa la Familia Takatifu mjini Kigali. Wakati huo walikuwa wamekomboa sehemu kubwa ya nchi na kuwafurusha watekelezaji wa mauaji ya kimbari. Hata hivyo makundi ya haki za binadaamu yanawatuhumu pia waasi kwa kutenda uhalifu, ambapo hakuna hata moja aliewajibishwa hadi wakati huu.
Picha: Alexander Joe/AFP/GettyImages
Mwisho wa mauaji ya kimbari
Julai 18 1994, kiongozi wa RPF Meja Jenerali Paul Kagame alitangaza kwamba vita dhidi ya wanajeshi wa serikali vimemalizika. Waasi walikuwa wakidhibiti mji mkuu na miji mingine muhimu. Awali waliiweka madarakni serikali ya mpito. Hatimaye Kagame alichukua hatamu ya urais kuanzia mwaka 2000 hadi sasa.
Picha: Alexander Joe/AFP/GettyImages
Makovu yasiyofutika
Mauaji yalidumu karibu miezi mitatu. Mara nyingi wahanga walichinjwa kwa mapanga. Majirani waliwauwa majirani. Si vichanga wala vikongwe waliohurumiwa na wauaji. Maiti na viungo vya mwili vilitapakaa mitaani kote. Hakuna familia ambayo haikuathirika. Si tu makovu ya kimwili kwa manusura yanayowakumbusha Wanyarwanda juu ya mauaji ya kimbari, kuna pia kihoro kikubwa.
Picha: Timothy Kisambira
Picha 121 | 12
Umoja wa Afrika mapema mwaka huu uliiomba Angola kuwa mpatanishi kati ya Rwanda na Congo chini ya mwamvuli wa chombo cha kikanda kinachojulikana kama Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Karibu watu 170,000 wameyakimbia makazi yao tangu M23 iliporejea mashariki mwa Congo, na kwenye mkutano huo wa kilele wa jana, wakuu hao walitoa mwito kwa wakimbizi wote kurejea kwenye mataifa yao, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya rais wa Congo.