1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda na DRC zachunguza kurudi kwa wapiganaji wa M23

11 Novemba 2021

Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Gen.Celestin Mbala Munsense amesema kwamba suala la wapiganaji wa M23 waliodaiwa kuishambulia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linachunguzwa.

Mai-Mai Milizen im Kongo
Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Jumapili iliyopita wapiganaji hao walishambulia vijiji kadhaa karibu na mji wa Bunagana na kusababisha wakaazi wengi wa eneo hilo kukimbilia Uganda.

Generali Celestin Mbala Munsense amesema hayo akiwa mjini Kigali, ambako amefanya mazungumzo na makamanda wa jeshi la Rwanda. Amesema kwamba suala hilo la shambulizi la waasi la usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, serikali za Rwanda na DRC zimeliachia tume ya uchunguzi katika mipaka ya nchi hizo, maarufu kama EJVM ambayo baadaye itatoa ripoti juu ya uchunguzi wake.

''Mpaka sasa tunaendelea kupata shutuma zenye mchanganyiko kutoka vyanzo mbalimbali, tumeamua kuliacha tatizo hilo lifuatiliwe na tume maalum ya nchi za maziwa makuu ili iweze kufanya utafiti na kutupa uhakika wa jambo lenyewe''.

Baada ya shambulizi hilo la Jumapili usiku, lawama za kila upande zilisikika baina ya Rwanda na Uganda kila upande ukitaja kwamba wapiganaji hao walitokea upande mwingine.

Je, M23 inaibuka tena?

This browser does not support the audio element.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Rwanda ilikanusha kuwepo kwa kitendo cha wapiganaji hao kutokea Rwanda. Jeshi la Rwanda RDF lilisema badala yake kwamba hizo zilikuwa ni propaganda za serikali ya Uganda kutaka kuharibu ushirikiano uliopo kwa sasa baina ya serikali za Kinshasa na Kigali.Kwa upande mwingine pia kundi la M23 lilitoa tangazo ambalo lilikanusha wao kuhusika katika shambulio hilo.

Watu wakiyakimbia makaazi yao mjini GomaPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Akiwa mjini Kigali, mkuu huyo wa jeshi la Kongo na ujumbe wa maafisa wakuu anaouongoza wamefanya pia mazungumzo na mkuu wa majeshi ya Rwanda Gen Jean Bosco Kazura katika makao makuu ya jeshi la Rwanda mjini Kigali.

Jenerali Munsense amesema kwamba eneo la maziwa makuu kwa ujumla limeendelea kukabiliwa na vitendo vya ughaidi na usalama mdogo unaosababishwa na makundi yenye silaha suala ambalo yeye anasema ushirikiano wa mataifa ndiyo unaweza kuweka kikomo kwa changamoto hizo.

''Ujumbe wangu uko hapa kujadiliana na wenzetu ni mipango gani tuichukue kama majirani ili kukabiliana na makundi ya kighaidi ambayo yanaendelea kuwa tishio la mataifa.Hii inakwenda na mwito wa umoja waafrika wa kuweka nguvu pamoja kukabiliana na vitisho vinavyozuia maendeleo yetu''.HRW: M23 walitumika kupambana na waandamanaji DRC

Amesema mazungumzo zaidi yamelenga kuhakikisha usalama kwenye mipaka ya nchi mbili suala ambalo litaendelea kuimarisha uhusiano wa nchi mbili.

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekuwa na historia ya migongano ya muda mrefu lakini ukurasa mpya wa uhusiano bora ulifunguliwa mwaka 2019 pale Rais wa Sasa wa DRC Felix Tshisekedi alipotwaa hatamu za uongozi nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW