Rwanda na Urusi zatuma wanajeshi Jamhuri ya Afrika ya Kati
21 Desemba 2020Msemaji wa serikali ya mjini Bangui amesema makundi matatu ya wapiganaji yamejaribu kuipindua serikali wiki moja kabla ya uchaguzi wa rais.
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Maxime Kazagui,ameliambia shirika la AFP leo juma tatu kwamba mamia ya wanajeshi wa Urusi wamewasili nchini humo ilikuzima jaribio la mapinduzi.
Kazagui amesema wanajeshi hao wa Urusi ambao wamekuja na silaha nzito, ni kulingana na ushirikiano wa kijeshi baina Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi hiyo. Aliendelea kusema kwamba wanajeshi wengine kutoka Rwanda tayari wamewasili na wameanza kupigana.
Wizara ya ulinzi ya Rwanda ilitangaza kwamba wanajeshi wake ambao wanashiriki katikakikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa,walishambuliwa na waasi wa rais wa zamani Francois Bozize. Na kwa hiyo serikali ya Rwanda iliamua kutuma wanajeshi wa ulinzi nchini humo kulingana na mkataba wa ulinzi kati ya Kigali na Bangui.
Makundi ya waasi yaungana na yaelekea Bangui
Hata hivyo idadi ya wanajeshi waliopelekwa huko Bangui na shughuli zao hazijulikani. Wizara ya ulinzi ya Rwanda inaelezea tu kwamba vikosi hivyo vitachangia kuhakikisha amani wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kuitishwa juma pili ya desemba 27.
Toka mwaka 2014 ,Rwanda ni miongoni mwa nchi zinazochangia wanajeshi wake katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).
Soma pia: Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kugombea uchaguzi ujao
Kikosi cha MINUSCA kina wanajeshi 11.500. Wanajeshi wa Rwanda wanahusika hasa na ulinzi a rais Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadera pamoja na Ikulu.
Ijumaa jioni, makundi matatu ya waasi wanaodhibiti theluthi mbili ya ardhi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza kujielekeza kwenye mji mkuu Bangui baada ya makundi hayo kutangaza kuungana pamoja.
Francois Bozize atuhumiwa kwa jaribio la mapinduzi
Mnamo Jumamosi serikali ilimtuhumu rais wa zamani Francois Bozize kwa jaribio la mapinduzi na kusema amewaunga mkono waasi hao. Chama cha Bozize kilikanusha tuhuma hizo.
Francois Bozize aliechukuwa madaraka mwaka 2003 kwa njia ya mapinduzi alipinduliwa kwa njia hiyo hiyo mwaka 2013. Baadae nchi hiyo iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Bozize alijitangaza kuwa mgomea wa urais kwenye uchaguzi wa Jumapili,lakini Korti ya Katiba ilitupilia mbali ugombeaji wake, kutokana na vikwazo alivyowekewa na Umoja wa Mataifa. Bozize ametuhumiwa na Umoja wa Mataifa kuyaunga mkongo makundi ya waasi ambayo yalifanya uhalifu wa kivita na uhalifu wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Rais Faustin Arc'Ange Touadera aliwambia wafuasia wake Jumamosi kwamba wanajeshi wake pamoja na wale wa Rwanda,Urusi na Kikosi cha Umoja wa Mataifa wanajipanga kukabiliana na uasi.
Duru za kiusalama zinaelezea kwamba wapiganaji mamluki wa mashirika ya kibinafsi kutoka Urusi walipambana na waasi hao kusini magharibi mwa mji mkuu Bangui.