1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda: Padri aliyegeukia siasa azuiwa Nairobi

24 Novemba 2016

Aliyewahi kuwa Padre wa kanisa Katoliki nchini Rwanda, ambaye kwa sasa amegeukia masuala ya siasa Thomas Nahimana amezuiwa kupanda ndege nchini Kenya ili kurejea nyumbani Rwanda.

Symbolbild - Ruanda Opfer des Bürgerkriegs
Picha: Getty Images/C. Somodeville

Kurejea kwa padri huyo wa zamani Thomas Nahimana baada ya miaka 11 ya kuishi uhamishoni nchini Ufaransa kunaibua mjadala nchini Rwanda ambako vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali vinamtuhumu padri huyo kutoa mahubiri yaliyochochea chuki za kikabila na kusababisha mauaji ya halaiki ya kabila ya Tutsi, mnamo mwaka 1994.

Padri Nahimana anapanga kurejea nchini mwaka Rwanda ambako amepanga kusajili chama kipya cha upinzani cha Ishema, na kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Padri Nahimana anasema, lengo kubwa la chama hicho ni kuwaunganisha tena watu wa Rwanda.

“Katika hali ya kushangaza, wakati tunajiandaa kupanda ndege mawakala wa shirika la ndege la Kenya walikuja na kutuzuia kupanda ndege ambayo ingeturejesha Rwanda” alisema Nahimana kwenye taarifa yake, huku akiapa kubakia katika uwanja wa ndege wa Nairobi hadi pale atakaporuhusiwa kuondoka, pamoja na wenziwe watatu. 

Mnamo mwaka 2011 Kanisa Katoliki nchini Rwanda liliiomba serikali ya Ufaransa kumzuia Nahimana kuandika makala zinazotoa madai yanayokanusha uhusika wake kwenye mauaji hayo ya halaiki ya mwaka 1994, ambapo makundi ya kabila ya Hutu yaliwauwa kiasi ya Watutsi 800,000 ndani ya siku 100 ya kusambaa kwa mauaji hayo.

Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Kagame anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu demokrasia nchini mwake. 

Padri huyo pamoja na mwenzake, Fortunatus Rudakema aliyeko nchini Italia, ambao wote ni wa kutoka kabila ya walio wengi ya Hutu walizindua tovuti inayoshambulia serikali ya rais Paul Kagame na kuwaenzi wahutu waliouwawa na wapiganaji wa chama chake tawala cha Rwandan Patriotic Front, RPF, ambacho awali kilikuwa kikundi cha waasi.

Kagame ametawala nchi hiyo ndogo iliyopo katika ukanda wa Afrika Mashariki tangu vikosi vyake vilipoweza kumaliza mauaji hayo ya halaiki ya kabila ya walio wachache ya Tutsi, na anataka kuchaguliwa tena katika uchaguzi utakaofanyika mwaka 2017, baada ya kubadilishwa kwa katiba ya nchi hiyo mwaka jana.

Huku mara zote akijitamba kwa kuimarisha ustawi na kuinua hali ya uchumi, Kagame mara nyingi amekuwa akikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa makundi ya haki za binadamu na mahisani wa Magharibi kwamba nchi hiyo haina uhuru wa kisiasa na kujieleza. Kikatiba Rwanda inatambulikana kuwa na siasa ya vyama vingi, ingawa kiuhalisia hakuna upinzani nchini humo.

Vyama vyote vya siasa vinayotambulika kwa ujumla wake vinaunga mkono maamuzi yatokanayo na sera za chama tawala cha RPF, tofauti na chama kimoja kidogo cha Democratic Green, ambacho ndicho pekee kilipinga mabadiliko ya katiba ya mwaka 2015, yanayomruhusu Kagame kusalia madarakani hadi mwaka 2034, iwapo atashinda uchaguzi. Hata hivyo chama hicho hakina mwakilishi bungeni.

Mwaka 2010, mmoja wa wapinzani nchini humo, Victoire Ingabire aliyeonyesha nia ya kugombea kwenye uchaguzi ujao, alitiwa kizuizini muda mfupi baada ya kurejea Rwanda akitokea uhamishoni. 

Mwandishi Lilian Mtono /AFPE/RTRE
Mhariri: Josephat Charo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW