1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda: Paul Kagame ameapishwa kuongoza muhula wa nne

11 Agosti 2024

Paul Kagame ameapishwa leo Jumapili kuhudumu muhula wa nne wa kuingoza Rwanda kwa miaka mingine mitano baada ya kushinda kwa zaidi ya asilimia 99 ya kura katika uchaguzi wa Rais wa Julai, 15.

Rwanda | Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Giscard Kusema

Viongozi kadhaa wa nchi na viongozi wengine kutoka mataifa ya Afrika waliungana pamoja kwenye sherehe za kuapishwa Rais wa Rwanda katika uwanja wa michezo wa kitaifa wa Amahoro wenye viti 45,000 mjini Kigali.

Kagame alikula kiapo mbele ya Jaji Mkuu Faustin Ntezilyayo, na ameahidi kulinda amani na mamlaka ya taifa na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Sherehe ya kuapishwa kwake imefanyika na kuhudhuriwa pia na maelfu ya Wanyarwanda waliofika uwanjani hapo tangu mapema leo asubuhi wakiwemo viongozi wa serikali na mashirika ya kiraia ambao pia walihudhuria hafla hiyo ya kuapishwa kwa Kagame mwenye umri wa miaka 66.

Ofisi ya msemaji wa serikali ya Rwanda ilitoa taarifa ikieleza kuwa, viongozi kadhaa barani Afrika walitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Soma Pia:  Changamoto zinazoukabili muhula mpya wa Kagame

Miongoni mwa viongozi hao ni Marais wa Kenya William Ruto, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Emmerson Mnagangwa wa Zimbabwe, Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini, Umaro Sissoco Embaló wa Guinea-Bissau, Nana Akufo-Addo wa Ghana.

Rais wa Rwanda Paul Kagame wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais 2024Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Wengine ni Marais wa Botswana Mokgweetsi Masisi, Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faure Essozimna Gnassingbé wa Togo, Mfalme Mswati III wa Eswatini na rais wa mpito wa Gabon Jenerali Brice Oligui Nguema.

Viongozi wengine waliowasili mjini Kigali kwa ajili ya kuhudhuria kuapishwa kwa Paul Kagame ni pamoja na Mkuu wa majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Makamu wa Rais wa Ivory Coast, Tiemoko Meyliet Koné, Rais wa Guinea, Mamadi Doumbouya na Waziri Mkuu wa Sao Tome, Patrice Trovoada.

Soma Pia: Kagame atetea rekodi ya Rwanda kuhusu demokrasia wakati wa kampeni 

Katika uchaguzi wa Rais wa Rwanda uliofanyika mnamo Julai 15 kiongozi wa chama cha Democratic Green Party, Frank Habineza alipata asilimia 0.5 tu na mgombea wa kujitegemea Philippe Mpayimana, alipata asilimia 0.32, kulingana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Wagombea hao waliopambana na Kagame katika uchaguzi wa mwaka 2017 ndio walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa mwaka huu baada ya viongozi kadhaa wa upinzani kuzuiwa.

Viongozi kadhaa wa barani Afrika wamempongeza Kagame kwa kupata fursa ya kuiongoza nchi yake kwa muhula wa nne, lakini wanaharakati wa kutetea haki wameitikia hatua hiyo kwa masikitiko.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Green Party, Frank HabinezaPicha: Guillem Sartorio/AFP/Getty Images

Baadhi ya wakosoaji hawakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa Rais uliomalizika nchini Rwanda, wamesema haukuwa huru na haki, lakini waangalizi wa uchaguzi akiwemo Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya David Maraga ambaye aliongoza ujumbe wa  maafisa 55 kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Bunge la Afrika Mashariki wameupongeza uchaguzi wa Rwanda.

Soma Pia: UN: Wataalamu wasema wanajeshi kati ya 3,000 na 4,000 wa Rwanda walipelekwa nchini Kongo 

Akizungumza mjini Kigali kuhusu uchaguzi wa rais wa Rwanda, katika wadhifa wake kama Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika masharikiJaji Mkuu mstaafu wa nchini Kenya David Maraga, amelisifu zoezi hilo kuwa la amani na utulivu. Amesema mchakato wa uchaguzi wa Rais nchini Rwanda ni mojawapo kati ya michakato bora aliyowahi kushuhudia.

Sifa na Ukosoaji 

Kagame, ambaye ameitawala Rwanda tangu mwaka 2000, anasifiwa kwa kuibadilisha nchi hiyo kiuchumi na kijamii, kwa kuijenga upya Rwanda kutoka katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, ambao yalisababisha vifo vya watu 800,000 lakini, uongozi wake umevutia sifa na ukosoaji, wa ndani na nje ya nchi.

Anasifiwa kwa kulijenga upya taifa lake lililosambaratika lakini pia analaumiwa kwa kutawala katika mazingira ambayo watu wana hofu, na pia kwa kuchochea ukosefu wa utulivu katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma Pia:Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya makundi ya waasi yanayojaribu kuipindua serikali DRC  

Rais Kagame amekabiliwa na shutuma nzito kutoka kwa Umoja wa Mataifa, Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoendelea kusababisha machafuko mashariki mwa DRC.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix TshisekediPicha: DW

Rwanda inakanusha vikali madai hayo na Rais Kagame amekuwa akiimarisha jeshi lake kwenye mpaka na  Kongo huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mvutano ambao waangalizi wa mambo wanahoji kuwa unatishia usalama na utulivu wa Ukanda wa Maziwa Makuu.

Chanzo: AFP