1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda yaadhimisha miaka 30 ya mauaji ya kimbari

8 Aprili 2024

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema jamii ya kimataifa haikuwajibika wakati wa mauaji ya kimbari yaliofanyika nchini humo mnamo mwaka 1994, huku akitoa heshima kwa wahanga 800,000 waliopoteza maisha yao wakati huo

Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, mnamo Aprili 7,2024
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: LUIS TATO/AFP

Miaka 30 baada ya mauaji hayo ya kimbari nchini Rwanda, raia nchini humo Jumapili walikusanyika katika mji mkuu Kigali huku wakibeba mishumaa kuwakumbuka waliouawa.

Kwa kuzingatia tamaduni, Rais Kagame aliweka mashada ya maua kwenye makaburi ya wahanga hao na kuwasha mwenge wa ukumbusho katika eneo la makumbusho ya mauaji hayo ambapo zaidi ya waathiriwa 250,000 wanaaminika kuzikwa.

Kagame asema Rwanda haitosahau mauaji ya kimbari

Akihutubia umati uliohudhuria hafla hiyo uliowajumuisha wakuu wa nchi za Afrika na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Rais Kagame alisema kuwa Rwanda ilifedheheshwa sana na ukubwa wa hasara iliyopata na kwamba mafunzo waliyopata yatakumbukwa daima.

Soma pia:Wiki ya kumbukumbu ya mauwaji ya kimbari nchini Rwanda

Rais Kagame aliongeza kuwa ni jamii ya Kimataifa iliyoshindwa kuisaidia nchi hiyo aidha kutokana na dharau ama uoga.

Rais Macron asisitiza kuhusu jukumu la Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda

Katika ujumbe aliotoa kupitia njia ya vidio, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisisitiza kuhusu maoni aliyotoa mnamo Mei 2021 wakati alipokiri kuhusu jukumu la Ufaransa katika mauaji hayo ya halaiki na kushindwa kuzingatia maonyo ya hatari ya mauaji hayo ya kimbari lakini hakuomba msamaha rasmi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: ISAAC FONTANA/EPA/picture alliance

Macro ameongeza kwamba anamshukuru Rais Kagame kwa kuyapokea vizuri maneno yake na kwamba hatua hiyo inafungua ukurasa mpya katika mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa  Halmashauri Kuu ya AU asema hakuna anayeweza kujitetea kwa kutowajibika wakati wa mauaji ya Rwanda

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema kuwa kushindwa kwa Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati, kumekuwa sababu ya aibu inayoendelea na kuongeza kwamba hakuna mtu hata Umoja huo wa Afrika unaoweza kujieteta kwa kutochukuwa hatua.

Soma pia: Ufaransa yaachia nyaraka za mauaji ya Rwanda

Faki aliongeza kuwa wanapaswa kuwa na ujasiri na kutambua hilo pamoja na kuwajibika.

Rwanda imeanza wiki moja ya maombolezo

Wakazi wengi waliohudhuria hafla hiyo waliliambia shirika la habari la AFP kwamba  wanashiriki historia hiyo ya kusikitisha ya nchi yao, na walipoteza wanafamilia kwenye mauaji hayo.

Hafla hiyo ya jana, iliadhimisha mwanzo wa wiki moja ya maombolezo ya kitaifa ambapo hakuna muziki unaoruhusiwa kupigwa katika maeneo ya umma ama redioni, huku matangazo ya televisheni yakihitajika kuzingatia kile kinachojulikana kama Kwibuka (kumbukumbu ya 30)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW