1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaadhimisha miaka 50 ya uhuru ''shingo upande''

2 Julai 2012

Rwanda imeadhimisha miaka 50 tangu ilipopata uhuru na maadhimisho hayo ambayo hayakuwa na shamra shamra kubwa yalifanywa sambamba na mengine ya miaka 18 tangu kusimamishwa kwa mauaji ya kimbari.

Rais Paul Kagame wa Rwanda
Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: picture-alliance/dpa

Uhuru wa Rwanda ulipatikana tarehe 1 Julai mwaka 1962, kutoka kwa wakoloni wa kibelgiji. Hata hivyo, kwa miaka mingi siku hiyo huadhimishwa shingo upande, kwani viongozi wa serikali na baadhi ya raia huamini kuwa uhuru huo hauna maana, kwani ulipatikana wakati wa mgawanyiko mkubwa ambao ulipelekea kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Mnamo miaka ya hivi karibuni, siku hiyo imekuwa ikijumuishwa na sherehe za siku ya ukombozi, tarehe 4 Julai, ambayo mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yalisimamishwa, na chama tawala kwa sasa, RPF, kuchukua hatamu za uongozi.

Siku kuu ya ukombozi hupewa umuhimu zaidi

Ruanda VölkermordPicha: AP

Hii ndo siku inayozungumzwa na serikali ya hapa bila chembe yoyote ya manung'uniko na hivyo inapewa umuhimu mkubwa.Sheikh Abdulkarim Harerimana ni mwanasiasa mkongwe nchini Rwanda anasema kuadhimisha siku ya ukombozi kuliko ile ya uhuru ni suala lililoanza hata abla ya serikali hii kuingia madarakani.

''Tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1973 yaliyofanywa na aliyekuwa rais wa Rwanda Habyarimana Juvenal, siku kuu ya uhuru iliambatanishwa na siku kuu ya mapinduzi hayo, ambayo ilifanyika tareke 5 Julai. Kwa hiyo siku ya mapinduzi hayo ilipewa uzito kuliko siku kuu ya uhuru kwa sababu Habyarimana alidai aliikomboa nchi kutokana na matatizo makubwa ya kisiasa''. Alisema Sheikh Harerimana.

Maadhimisho bila shamra shamra

Flash-Galerie Ruanda Versöhnung Bild 2Picha: James Nzibavuga

Ingawa kila mwaka siku ya uhuru haipewi uzito mkubwa kama ile ya ukombozi. Mwaka huu hali ni tofauti kidogo angalau yanaonekana maandalizi ya hapa na pale, pengine kwa sababu sababu sasa maadhimisho ni ya nusu karne. Alipoulizwa iwapo Rwanda itasherehekea miaka huo tangu kuondoka kwa wakoloni, rais wa Rwanda Paul Kagame alisema itaadhimishwa ''kwa namna fulani'', pengine ili kutoa nafasi ya kuutafakari uhuru huo.

Ijapokuwa wengi hawapendi kutoa maoni yao waziwazi lakini wanapendekeza kwamba siku ya uhuru iwe inapewa umuhimu mkubwa kwa kuwa inasalia kuwa na hadhi yake kama siku ya uhuru wa taifa.

Mwandishi: Sylvanus Karemera/Dw-Radio-Kigali

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW