1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaanza kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola

Benjamin Kasembe9 Desemba 2019

Rwanda yaanza kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola

Kongo Impfung gegen Ebola in Mbandaka
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Serikali ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zimezindua kampeni ya pamoja ya kutoa chanjo ya homa ya Ebola. Chanjo hiyo ilianza kutolewa jana mjini Rubavu nchini Rwanda. Hayo yanajiri wakati ambapo shirika la madaktari wasio na mpaka wiki iliyopita likitangaza kuondoka kwenye jimbo la Ituri kutokana na mashambulizi yanayofanywa dhidi ya vituo vyake kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa Ebola. 

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema katika kipindi cha mwaka mmoja raia laki mbili kwenye wilaya ya Rubavu na Rusizi nchini Rwanda watapewa chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Kimarekani ya Johnson & Johnson na wengine zaidi ya 500, 000 wanasubiri kupewa chanjo hiyo hapa mkoani Kivu.

Mmoja wa maafisa wa WHO nchini Kongo, Ibrahim Sose, amepongeza ushirikiano huo kati ya mataifa haya mawili katika juhudi za kukabiliana na janga hili hatari.

Hata hivyo, mratibu wa kikosi cha kupambana na Ebola hapa nchini Kongo Dokta Jean Jacques Muyembe, amesema kwa kushirikiana na nchi ya Rwanda itakua sasa rahisi kuitokomeza homa ya Ebola inayoendelea kuyagarimu maisha ya wakaazi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Muyembe ameiambia DW kwamba hakutashuhudiwa tena idadi kubwa ya vifo iwapo ugonjwa wa Ebola utazuka kwa mara nyingine katika siku zijazo.

Kampeni ya kuutokomeza ugonjwa wa Ebola unaendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Kwa upande wao wakaazi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wameelezea mtazamo wao kuhusu kampeni hii ya chanjo ya Ebola na hapa wanaeleza zaidi.

Wakati hayo yakiendelea shirika la madaktari wasiokua na mipaka MSF limetangaza kusitisha shughuli zake mkoani Ituri tangu wiki iliyopita kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wafanyakazi wake ambao wamekuwa wakipambana kuutokomeza ugonjwa wa Ebola.

Hali hii imesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia katika maeneo hayo ambao wameanza kupoteza matumaini ya kupewa matibabu ya homa ya Ebola kutokana na tangazo hilo la MSF. Kwa zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa Ebola imeongezeka na kufika 2,209 tangu mwezi wa Agosti mwaka jana. Benjamin Kasembe, DW, Goma.