Rwanda yaanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola kwa hiari
9 Desemba 2019Rwanda imeanza kutekeleza mpango wa kutowa chanjo ya Ebola kwa hiyari katika maeneo ya mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Hatua hiyo inalenga kuzuia kuenea kwa virusi vya maradhi ya Ebola kutoka nchi hiyo jirani ya Kongo.
Waziri wa Afya wa Rwanda, Diane Gashumba akizungumza na waandishi habari jana amesema nchi zote zilizoko kwenye maeneo hatarishi hata ikiwa hakikukabiliwa na Ebola zimeshauriwa na Shirika la Afya Duniani, WHO kutumia chanjo mpya iliyotengenezwa na kampuni ya kimarekani ya Johnson & Johnson.
Waziri huyo amesema kwamba fikra nyuma ya mpango huo ni kuwalinda wale walioko kwenye nafasi kubwa ya kuingiliana na watu wanaoishi kwenye maeneo ambako ugonjwa wa Ebola umeripotiwa kuwepo.
Ulikoanzia mripuko wa Ebola nchini Kongo ambako zaidi ya watu 2,200 wamefariki tangu Agosti mwaka 2018 ni kilomita 350 kutoka kaskazini mwa Goma katika eneo la Beni na Butembo.