1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaanza kutoa chanjo ya COVID-19

15 Februari 2021

Rwanda imeanza zoezi la kutoa chanjo ya virusi vya corona kwa wananchi wake wiki moja baada ya wakazi wa mji mkuu wa nchi hiyo Kigali kuondoka katika zuio la kukaa ndani.

AstraZeneca - Impfstoffhersteller
Picha: Frank Hoermann/Sven Simon/imago images

Zoezi la kuitoa chanjo hiyo limetangazwa kwa umma na wizara ya afya nchini Rwanda na imeanzia kutolewa kwa makundi yaliyo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19. Hata hivyo, wizara hiyo haikutangaza ni kiasi gani cha chanjo inayotolewa na idadi ya watu wanaotakiwa kuchanjwa kwa muda fulani.

Lakini imesema kwamba watu wenye hatari ya kupata maambukizi kwa urahisi ndiyo wameanza kuchanjwa kama vile wahudumu wa afya pamoja na wafanyakazi wote walioko kwenye sekta ya afya hasa wale wanaowahudumia wagonjwa wa virusi vya corona.

Waziri wa Afya wa Rwanda, Dokta Daniel Ngamije kupitia ukurasa wake wa Twitter amethibitisha kutolewa kwa chanjo hiyo, lakini alijizuia kutoa majibu mwa maswali haya yote.

Soma zaidi: Afrika Kusini yasitisha kuanza utoaji chanjo ya AstraZeneca

Hata hivyo, mwezi uliopita alipokuwa akizungumza na televisheni ya taifa Dokta Ngamije alisema kwamba Rwanda ilitegemea kupokea chanjo zaidi ya milioni moja zikiwemo zile aina ya AstraZeneca na Pfizer ifikapo mwezi wa pili katikati na kwamba pindi tu zitakapofika wizara ya afya itaanza kazi ya kuitoa chanjo hiyo.

Mfanyakazi katika kituo cha afya cha Gashora, RwandaPicha: picture-alliance/Xinhua/C. Ndegeya

''Tutazipokea chanjo hizo na tumeshayaandaa ya kuitoa kwa wananchi kwa sababu tayari tuna uwezo wa kuzihifadhi kutokana na aina ya kila chanjo,'' alifafanua Dokta Ngamije.

Lakini kwa sasa wizara ya afya ya Rwanda imeshindwa kutangaza ni aina gani ya chanjo ambayo imeanza kutolewa na tayari ni watu wangapi mpaka sasa wamechanjwa. Hali hii imezua maswali miongoni mwa baadhi ya wananchi.

Kupitia tangazo lililotolewa kwa umma, wizara ya afya imesema kwamba chanjo hizo zimepatikana kutokana na kile ilichokijata kama ushirikiano wa kimataifa na kwamba chanjo zimekidhi viwango vya ubora kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO.

Wizara hiyo imesema kupitia Umoja wa Afrika, Rwanda inatazamiwa kupokea chanjo zaidi na ndipo itakapoanza chanjo ya wazi kwa wananchi wote.

Mpaka sasa zaidi ya watu 17,000 nchini Rwanda wameambukizwa virusi vya corona, huku wengine 239 wakiwa wamepoteza maisha yao kutokana na janga la COVID-19.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW